Waziri wa Maji, Mhe.Jumaa Aweso,akitoa maelezo mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa makubaliano kati ya Wizara ya Maji kupitia Idara ya Rasilimali za Maji na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA),hafla iliyofanyika leo Februari 2,2022 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Clement Kivegalo (kulia) na Mkurugenzi wa Rasiliamali za Maji Dk.George Lugomela,wakisaini makubaliano kati ya Wizara ya Maji kupitia Idara ya Rasilimali za Maji na RUWASA ya utaratibu wa wa utekelezaji wa miradi ya mabwawa ya maji kwenye maeneo yanayosimamiwa na RUWASA leo Februari 2,2022 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Clement Kivegalo (kulia) na Mkurugenzi wa Rasiliamali za Maji Dk.George Lugomela,wakibadilishana Mkataba baada ya kusaini makubaliano kati ya Wizara ya Maji kupitia Idara ya Rasilimali za Maji na RUWASA ya utaratibu wa wa utekelezaji wa miradi ya mabwawa ya maji kwenye maeneo yanayosimamiwa na RUWASA leo Februari 2,2022 jijini Dodoma.
…………………………………………..
Na.Alex Sonna,DODOMA
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amezitaka taasisi za Bodi za Maji za Mabonde na Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha zinasimamia utekelezaji wa makubaliano yao kuhakikisha yanaleta matokeo chanya kwa wananchi.
Hayo ameyasema leo Februari 2,2022 jijini Dodoma baada ya kushuhudia utiaji saini wa makubaliano kati ya Wizara ya Maji kupitia Idara ya Rasilimali za Maji na RUWASA ya utaratibu wa wa utekelezaji wa miradi ya mabwawa ya maji kwenye maeneo yanayosimamiwa na RUWASA.
Aweso amesema kuwa Wizara ya Maji imefanya mageuzi makubwa ya kisekta kwa dhumuni la kufikisha huduma ya maji mijini na vijijini, ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko ya uongozi wa Wakala wa Ujenzi wa Mabwawa na Uchimbaji wa Visima (DDCA) kwa sababu ya kutofanya vizuri kwa muda mrefu.
“Maridhiano haya yananipa matumaini ikiwa na hatua ya kuimarisha eneo la ujenzi wa mabwawa ambalo tumekuwa hatufanyi vizuri kwa miaka mingi na yamekuja wakati muafaka baada ya Serikali kuwekeza Sh. bilioni 139.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji na ununuzi wa mitambo ya ujenzi wa mabwawa, uchimbaji wa visima na utafiti wa maji itakayoongeza ufanisi kwa Bodi za Maji za Mabonde, RUWASA na DDCA”, Aweso amesema.
Hata hivyo amesisitiza kuwa anatarajia kuona uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kwenye ujenzi wa mabwawa unazaa matunda, huku akielekeza kuwa mabwawa yote yanayojengwa ni lazima yazingatie viwango na thamani ya fedha ili kuleta tija kwa wananchi.
Aweso amesema jukumu la wizara hiyo ni kuhakikisha rasimali za maji zinavunwa na kuhakikisha watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama.
Aidha Waziri Aweso amesema atosita kuwachukulia hatua maafisa mabonde ya maji watakaobainika kufanya ubadhilifu katika miradi ya maji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Clement Kivegalo amesema kuwa hatua ya makubaliano hayo ni utekelezaji wa muongozo alioutoa Waziri wa Maji unaotaka taasisi zote za Wizara ya Maji kushirikiana kwa pamoja bila kujali mipaka au vyeo vyao kwa maslahi ya sekta.
Naye Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji Wizara ya Maji, Dkt. George Lugomela amesema miongoni mwa vipengele vya makubaliano hayo ni kazi za utafiti, uchoraji wa ramani na makadario ya gharama za ujenzi zitafanywa na Bodi za Maji za Mabonde huku kazi za ujenzi zikifanywa na RUWASA pamoja na kushirikiana katika usimamizi, ulinzi na utunzaji wa vyanzo vya maji.