……………………………………………………………
Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Mhe. David Concar kwa lengo la kuendeleza ushirikiano na Uingereza katika kuwezesha na kukuza Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na Uingereza.
Akiongea na Balozi wa Uingereza Ofisi za Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mtumba, Dodoma, Waziri Kijaji amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Uingereza kutekeleza maazimio ya Mkutano wa Serikali kwa Serikali (G2G) kati ya Serikali ya Tanzania na Uingereza yalioyolenga kuboresha mazingira ya Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza.
Naye, Balozi Concar amesema kuwa Serikali ya Uingereza itaendelea kutekeleza maazimio hayo kwa kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza mpango kazi jumuishi unaolenga kuziwezesha taasisi za umma na binafsi zinazohusika na Uwekezaji na Biashara kupanga vipaumbele vya kibiashara vinavyotekelezeka kwa kuzingatia mabadiliko mbalimbali yanayoweza kujitokeza.
Kongamano la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza lilifanyika Novemba 16, 2021, Dar es salaam na lililenga kupanua zaidi wigo wa ushirikiano katika maeneo ya biashara na uwekezaji hususan sekta za nishati, madini, miundombinu, kilimo, uchumi wa bluu na utalii, kuhamasisha wafanyabiashara wa Uingereza kuja kuwekeza nchini na wafanyabiashara wa Tanzania kuuza bidhaa zao Uingereza.