************************
Na Mwandishi wetu, Mihambwe
Wauguzi wa Zahanati ya Mihambwe iliyopo Kata ya Mihambwe Tarafa ya Mihambwe wamepongezwa kwa kuongoza wa kwanza kiwilaya kwa wingi wa utoaji wa huduma ya chanjo ya Uviko 19 kwa Watu.
Hayo yamebainishwa Leo Jumanne Februari 1, 2022 wakati wa ziara iliyofanywa na Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu kwenye Zahanati ya Mihambwe ambaye alienda kuwapongeza Wauguzi na kusikiliza changamoto zinazowakabili kwa ajili ya kuzipatia utatuzi.
“Kwanza Serikali tunawapongeza kwa utoaji wa huduma bora nyakati zote. Pili sio kwa umuhimu, Serikali tunawapongeza kwa uongozaji kiwilaya uchanjaji chanjo ya Uviko 19 (Corona 19) ambapo Zahanati ya Mihambwe mmekuwa wa kwanza kiwilaya, mmechanja jumla ya Watu 1405 na anayefuata amechanja Watu 342. Hongereni sana, nawasihi muendelee kuwa bora zaidi.”
“Pia nawapongeza Wananchi wa Tarafa ya Mihambwe kwa kuhitikia na kuunga mkono kivitendo wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kuchanja chanjo ya Uviko 19 kwa hiyari yao.” Alisema Gavana Shilatu.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Dk. Merkezedek Liyama alishukuru kwa kuona mchango wa utendaji kazi wao umeonekana na kuthaminiwa.
“Sisi tunashukuru kwa kuyaona yale tunayoyafanya na tunahaidi kuendelea kupambana kutoa huduma bora pasipo kuchoka.” Alisema Dk. Liyama
Tarafa ya Mihambwe ina Zahanati 5 na Kituo cha Afya kimoja ambacho kipo hatua ya ukamilishwaji kujengwa tayari kuanza huduma.
Katika ziara hiyo ya kutembelea Zahanati ya Mihambwe, Gavana Shilatu aliambatana na Mtendaji Kata Mihambwe na kuhaidi kutatua changamoto zinazowakabili.