Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akisoma taarifa ya miezi mitatu kwa waandishi wa habari mjini Babati.
*****************************
Na Mwandishi wetu, Babati
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Manyara, imepokea malalamiko 57 ya uchunguzi wa mashtaka, kwenye kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Mkuu wa TAKUKURU wa mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu, ameyasema hayo ofisini kwake mjini Babati wakati akizungumzia taarifa ya TAKUKURU ya miezi mitatu ya kutoka Oktoba hadi Desemba mwaka jana.
Makungu ameeleza kuwa kati ya malalamiko hayo 57 yaliyopokelewa kwenye kipindi hicho cha miezi mitatu, malalamiko 19 yalikuwa yanahusiana na rushwa.
Amesema malalamiko hayo 57 malalamiko matano yanahusiana na idara ya elimu kwenye halmashauri zote saba za mkoa huo na malalamiko dhidi ya polisi ni matatu.
Amesema malalamiko dhidi ya wenyeviti, watendaji wa vijiji na kamati mbalimbali za vijiji malalamiko 33, idara ya afya malalamiko manne, watu binafsi na mashirika binafsi manne.
“Malalamiko mengine yametolewa kwenye idara ya mahakama matatu, mashirika ya dini moja, vyama vya ushirika, wakala wa barabara za vijijini na mijini (Tarura) na idara ya maliasili matatu,” amesema Makungu.
Amesema kati ya malalamiko hayo 57, malalamiko 19 hayahusiani na vitendo vya rushwa hivyo wahusika walishauriwa ipasavyo na yale yanayohusu rushwa yapo kwenye hatua ya uchunguzi.
“Katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba mwaka jana, kesi nane zimefunguliwa mahakamani na kufanya jumla ya kesi zinazohusiana na mahakama kuwa 33,” amesema Makungu.