Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija akisaini kitabu cha wageni walipowasili pamoja na wenzake katika Mradi. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC)-Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu na katikati ni Mhandisi Daniel Wambura, Afisa Afya na Usalama Mahala Pa Kazi (OSHA).
Muonekano wa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania yanayoendelea kujengwa ambapo kwa mujibu ya taarifa ya Wakandarasi wa majengo haya yatakamilika ifikapo Desemba mwaka huu.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania umefikia asilimia 50 ya ujenzi hatua ambayo inaelezwa kuwa ifikapo mwezi Desemba mwaka huu Mradi huu utakuwa umekamilika kwa asilimia 100 na kuwa tayari kwa matumizi.
Akizungumza na baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania waliofanya ziara leo tarehe 01 Februari, 2022 katika Mradi huo uliopo katika eneo la Tambuka Reli jijini Dodoma, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bw. Solanus Nyimbi alisema kuwa kwa sasa hatua kubwa ya ujenzi wa majengo hayo ‘structures’ imeshafanyika hivyo hatua inayofuata ni ya umalizaji ‘finishing’.
“Wahe. Majaji kwa sasa hatua kubwa ya ujenzi wa majengo katika mradi huu imeshafanyika, hivyo hatua inayofuata ambayo tunaamini na tumehakikishiwa ni kuwa ifikapo Desemba mwaka huu, mradi huu wa ujenzi utakuwa umekamilika,” alisema Bw. Nyimbi.
Naye; Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Augustine Mwarija akizungumza kwa niaba ya Majaji wenzake waliofanya ziara kwenye mradi huo alisema kuwa wamefurahi kuona jengo hilo ambalo wameelezwa limefikia asilimia 50 na wameridhishwa na hatua iliyofikiwa.
“Tumekagua jengo tumeliona na tumeambiwa kuwa ifikapo mwezi Desemba litakuwa limekamilika, hivyo tumeridhika na hatua iliyofikiwa hadi sasa,” alisema Mhe. Jaji Mwarija.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi kwenye Mradi huo tarehe 26 Januari, 2022, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa mradi huo unategemea kugharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania billioni 129.7.
Jengo hilo la Makao Makuu ya Mahakama linajumuisha Mahakama ya Juu/Upeo (Supreme Court), Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu (Masijala Kuu) na lina ukubwa wa mita za mraba 60, 000.