****************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema Serikali inaendelea kujenga na kuboresha mazingira bora ya wawekezaji ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na zitakazoweza kushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Aidha mkoa huo umeahidi kukabili changamoto ya umeme kwenye kiwanda kikubwa Afrika Mashariki kinachotengeneza matenki ya kusafirishia mafuta cha Aluminum Trailers Ltd kilichopo Picha ya Ndege wilayani Kibaha.
Ahadi hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alipotembelea kiwanda hicho na viwanda vingine vya uzalishaji mitungi ya gesi, matenki na mabomba ya maji, kiwanda cha chuma chuma, kiwanda cha uzalishaji jipsam na boti ambavyo vyote viko chini ya kampuni ya Lake Group, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea viwanda mkoani humo ili kujua mafanikio na changamoto zinazowakabili wawekezaji kwenye viwanda.
Kunenge alisema kuwa umeme bado ni changamoto kwani umekuwa ukikatika mara kwa mara lakini mkoa utahakikisha changamoto hiyo inaondoka ili wawekezaji wasipate usumbufu wakati wa uzalishaji.
“Niliwaelekeza watu wa Tanesco kupitia viwanda vyote ndani ya mkoa ili kujua mahitaji yao ya umeme hasa wale wenye matumizi makubwa ili wapewe kipaumbele kwa kuwa na umeme wao na changamoto ya hapa itapatiwa ufumbuzi ili kazi zifanyike kwa ufanisi,”alisema Kunenge.
Alieleza, tayari wamewasiliana na waziri husika na pia hata Rais akiwa Mkuranga aliahidi kusaidia mkoa wa Pwani kuwezeshwa kwenye miundombinu mbalimbali ikiwemo ya nishati, maji na barabara kutokana na kuwa ni moja ya mikoa inayoongoza kwa kuwa na viwanda vingi.
“Nimatarajio yetu tatizo hili litakwisha kwani jitihada bado zinafanyika na mkoa utaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji ili kuwaondolea changamoto zinazosababisha washindwe kufikia malengo yao,”alisema Kunenge.
Akimkaribisha mkuu wa mkoa ofisa mwajiri na rasilimali watu wa kiwanda hicho cha Aluminum Hussein Ally alibainisha kwa mwezi wanazalisha matenki 15 na wametoa ajira kwa watu zaidi ya 90.
Ally alisema kuwa hadi sasa kiwanda hicho kimeshazalisha matenki 95 na mbali ya kuuza hapa nchini pia wanauza nje ya nchi ambapo kampuni yao inatengeneza matenki hayo ya mafuta kwa kutumia Aluminum.
Naye ofisa mwajiri wa Lake maeneo ya Visiga na Madafu Fadhil Msemwa Alifafanua viwanda hivyo vimetoa ajira rasmi za watu 400 wakiwemo wanaotoka maeneo ya mkoa wa Pwani na maeneo jirani ya mkoa huo.