Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Nishati na Maji (EWURA) Mhandisi Godfrey Chibulunje,akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 1,2022 jijini Dodoma (hawapo pichani) wakati akitangaza bei mpya za mafuta.
………………………………………………………
Na.Alex Sonna,DODOMA
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kupungua kwa bei ya mafuta ya taa kwa Sh.44 na Petroli Sh. 21 katika Bandari ya Dar es salaam huku ikianzisha bei ya kikomo na bei ya chini ambazo zitaanza kutumika kesho.
Hata hivyo, kwa upande wa mafuta ya Dizeli Bei itaongezeka kwa Sh.13 kwa lita kwenye Bandari hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Godfrey Chibulunje, ameyasema hayo Leo Februari 1,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Amesema hatua hiyo inatokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia ambapo bei za rejareja za mafuta ya Petroli na Dizeli kwa Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) zimepungua kwa Sh.123 lita (petroli) na Sh.92 (dizeli).
“Bei za rejareja za mafuta ya petroli na dizeli kwa Mikoa ya Kusini ambayo ni Mtwara, Lindi na Ruvuma zinaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la Januari 5, mwaka huu na hii ni kwasababu kwa mwezi Januari hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia Bandari ya Mtwara,”amesema.
Kuhusu bei ya kikomo na ya chini, Mhandisi Chibulunje amesema katika kuhakikisha kunakuwa na ushindani sawa bei hizo zitaanza kutumika kesho hivyo ununuaji wa mafuta kutoka kwenye maghala sasa ni bei mbili na muuzaji hatatakiwa kuzidisha.
“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei ya kikomo au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa kama ilivyokokotolewa kwa kutumia fomula na kanuni za kupanga bei za mafuta za mwaka 2022,”amesema.
Amebainisha kuwa katika bei ya kikomo ya mafuta ya petroli Sh. 2,350.54 (Petroli), Sh. 2,208.51(Dizeli) na Sh. 2.161.76(Mafuta ya Taa) kwa Bandari ya Dar es salaam huku bei za chini zitakuwa Sh. 2,227.54(Petroli), Sh. 2,085.51 (Dizeli) na Sh. 2,038.76 (Mafuta).
Aidha, amesema katika kufuatilia mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia, kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa bei ya mafuta kwa Mwezi Machi na Aprili, mwaka 2022.
“Hata hivyo, EWURA itaendelea kufuatilia mwenendo huo kwa karibu ili kuishauri serikali hatua za kuchukua katika harakati za kupunguza makali ya bei ya mafuta,”amesema.