Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza katika kikao na Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) kilichofanyika katika ofisi za mamlaka hiyo, jijini Arusha.
Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akitoa malekezo katika kikao na Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) kilichofanyika katika ofisi za mamlaka hiyo, jijini Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA), Mhandisi Justine Rujomba akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba.
………………………………………………………………….
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba ameitaka Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA) kuhakikisha miradi yote ya maji inayotekeleza inakamilika kwa wakati.
Naibu Katibu Mkuu Kemikimba ametoa maelekezo hayo baada ya kupokea taarifa ya hali ya utendaji wa mamlaka kwa mwaka wa fedha 2021/22 kufika mwezi Disemba, 2021katika kikao na menejimenti hiyo kilichofanyika katika ofisi za mamlaka hiyo jijini Arusha.
Mhandisi Kemikimba amesema AUWSA ina jukumu la kukamilisha miradi yote ya maji wanayoitekeleza iliyo ndani na nje ya maeneo inayotoa huduma kulingana na mikataba na kutakuwa hakuna nyongeza ya muda kwa mradi wowote.
“Mnafanya kazi nzuri lakini lazima muongeze kasi ya kazi, kama kuna changamoto zozote zilizo nje ya uwezo wenu mtupe taarifa tuzitatue haraka. Pia, menejimenti muhakikishe mnaimarisha utendaji wenu kwa kuwa utekelezaji wa miradi wa maji ni suala linalopaswa kupewa umuhimu mkubwa”, amesema Naibu Katibu Mkuu.
Mkurugenzi wa Usambazaji Majisafi na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Maji, Joyce Msiru ameisisitiza mamlaka kuhakikisha kuwa kazi zote zinazowezekana kufanyika kwa sasa zifanyike wakati wakisubiri utaratibu, vibali au maelekezo maalum kwa kazi nyingine ili kuokoa muda wa utekelezaji.
Amesisitiza kuwa kwa sasa hakuna changamoto ya upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hati zote za madai zinalipwa kwa wakati kulingana na kila hatua ya utekelezaji wa miradi.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA), Mhandisi Justine Rujomba alisema kuwa utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Jiji la Arusha ulikuwa umefikia Asilimia 80.
Aidha, Mamlaka inaendelea kusimamia na kutekeleza miradi ya Force Account katika Maeneo ya Mirerani, Enguik-Monduli, Mageri-Ngorongoro, Ayalabe na Bwawani-Karatu, Namanga pamoja na Oldonyosambu na iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Ameongeza kuwa mataraijio ya mamlaka ni kuongeza mtandao wa majisafi kwa zaidi ya kilomita 453.829 katika maeneo mbalimbali.
“Lengo ni kuongeza kilomita 200 jiji la Arusha, kilomita 30.561 mji wa Ngaramtoni, kilomita 95 mji wa Monduli, kilomita 73.268 mji wa USA River na kilomita 55 mji wa Longido. Ongezeko hili la mtandao litapelekea huduma ya majisafi kuongezeka kutoka asilimia 69.8 ya sasa na kufika asilimia 95.”, amefafanua Mhandisi Rujomba.
Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Arusha imeongezeka kutoka wastani wa asilimia 53 mwaka 2020 na kufikia asilimia 69.8 mwezi Disemba 2021, huku mtandao wa majisafi ukifikia 1,165.5km, lengo ni kufikia 1,185.4 km jijini Arusha ifikapo mwezi Juni 2022.