Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhandisi Hamad Masauni,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao chake na uongozi wa ngazi ya juu wa Jeshi la polisi ili kutoa mrejesho wa matokeo ya kilichojadiliwa kuhusu kadhia ya matukio ya mauaji yanayoendelea nchini kilichofanyika leo Januari 31,2022 jijini Dodoma.
……………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
ZAIDI ya watu 150 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini kutokana na tuhuma za mauaji katika maeneo mbalimbali nchini kwa kipindi cha mwezi mmoja huku Mikoa vinara wa matukio ya mauaji ni Kagera, Dodoma,Mara,Tabora na Kigoma.
Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeunda kamati ya kuishauri Serikali kuhusu namna ya kufanya katika kupata suluhisho la kudumu katika kuzui uhalifu na mauaji yaliyokithiri nchini huku ikitoa siku 21 kukamilisha kazi yake na kurudisha mrejesho kwenye wizara hiyo.
Hatua hiyo imekuja kufuatia hivi karibuni kushamiri kwa matukio ya watu kuuana huku Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango akitoa siku saba kwa Jeshi la polisi nchini na idara zake zote kutafuta ufumbuzi wa mauaji yanayoendelea nchini.
Hayo yameelezwa leo Januari 31,2022 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Hamadi Yusuphu Masauni wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kupokea mrejesho kwa viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi nchini juu ya mauaji yanayoendelea kutokea nchini.
Waziri Masauni amesema kutokana na kukithiri vitendo vya mauaji nchini hadi sasa Jeshi la polisi linawashikilia watu zaidi ya 150 huku akitaja mikoa vinara kwa mauaji kuwa ni Kagera, Dodoma,Mara ,Songwe,Tabora na Kigoma.
Amesema matukio hayo ni kuanzia Januari mosi hadi 31 mwaka huu ambapo amedai kesi hizo zipo katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka,Mahakamani na zingine zipo katika upelelezi.
Ametaja sababu mbalimbali za mauaji hayo kuwa ni pamoja na imani za kishirikina,wivu wa mapenzi,wivu wa maendeleo,visasi,migogoro ya ardhi,mali na ulevi na kueleza kuwa Serikali haiwezi kukaa kimya na kudharau malalamiko ya wananchi .
Katika hatua nyingine,Waziri Masauni ameunda Kamati ya kuishauri Serikali nini kifanyike ili kupata suluhisho lakudumu la matatizo hayo ambapo ndani ya siku 21 ije na Mkakati wa Kitaifa kuhakikisha wanadhibiti changamoto hiyo.
Amesema kuundwa kwa kamati hiyo kutasaidia kupatikana kwa suluhisho la kudumu katika kuzuia mauaji na uhalifu mwingine nchini huku akitaka watanzania kutoa ushirikiano katika kuwabaini wahalifu.
Masauni amesema,kamati hiyo itahusisha jopo la wataalam kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi,Tamisemi,Jeshi la Polisi,Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali,Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Usalama wa Taifa,Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka,Takukuru,Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,na Elimu ya juu.
Katika hatua nyingine Waziri Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha wahusika wa mauaji ambao hawajakamatwa katika maeneo mengine wanakamatwa mara Moja.
Ametaja sababu mbalimbali za mauaji hayo kuwa ni pamoja na imani za kishirikina,wivu wa mapenzi,wivu wa maendeleo,visasi,migogoro ya ardhi,mali na ulevi na kueleza kuwa Serikali haiwezi kukaa kimya na kudharau malalamiko ya wananchi .