Katibu wa Bunge, Ndg. Nenelwa Mwihambi, akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma kuhusu kukamilika kwa zoezi la uteuzi na utaratibu wa Uchaguzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
……………………………….
Na.Alex Sonna,DODOMA
KATIBU wa Bunge na msimamizi wa uchaguzi wa Spika Nenelwa Mwihambi(NDC) ametangaza kukamilika zoezi la uteuzi na utaratibu wa uchaguzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania leo Januari 31,2022 saa 10.00 jioni.
Akiongea na Waandishi wa habari Leo Bungeni Dodoma,amesema zoezi hilo liliruhusu Wagombea ambao ni wabunge na wasio wabunge na kwamba kwa wagombea wenye vyama,vyama vyao vilitakiwa kuwasilisha majina yao kwenye tume ya uchaguzi.
Amesema hadi sasa majina ya wagombea yaliyowasilishwa na kukidhi matakwa ya kisheria ni tisa ambapo miongoni mwa wagombea hao,nane sio wabunge na mmoja ni mbunge.
Sambamba na hayo ameyataja majina ya wagombea hao kuwa ni Abdullah Mohammed Said (NRA),Ivan Jackson Maganza (TLP),David Daud Mwaijojele (CCK),Georges Gabriel Busungu (ADA-Tadea),na Kunje Ngombale Mwiru.
Wengine ni Maimuna Said Kassim (ADC),Ndonge Said Ndonge (AAFP),Saidoun Abrahman Khatibu (DP) na Tulia Ackson(CCM).
Aidha Katibu huyo wa Bunge amewataka wagombea hao kufika mapema Bungeni hapo kesho na kwamba saa tatu asubuhi au muda mfupi baada ya hapo atawasilisha majina yao mbele ya wapiga kura ambao ni waheshimiwa wabunge .
Ametumia pia nafasi hiyo kuwashukuru wagombea wa vyama vyote vya siasa waliojitokeza ikiwa ni pamoja na kuipa ushirikiano wao Ofisi hiyo ya Katibu wa Bunge hadi zoezi hilo linakamilika