************
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kesho tarehe 1 Februari, 2022 itaanza rasmi kampeni ya kukagua walipakodi wasiotoa risiti za EFD kila wanapouza bidhaa na huduma mbalimbali na wanunuzi wasiodai risiti hizo kila wanapofanya manunuzi.
Kampeni hiyo endelevu itafanyika nchi nzima na itahusisha kukagua wafanyabiashara wote wanaostahili kutoa risiti na hawafanyi hivyo, wanunuzi wasiodai risiti za EFD, kuhamasisha pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa risiti hizo kwa maendeleo ya kila mtanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo, amesema kuwa, kampeni hiyo imelenga kujenga utamaduni wa kutoa na kudai risiti za EFD kila baada ya mauzo na manunuzi.
“Kampeni hii inawahusu wote yaani wauzaji na wanunuzi wa bidhaa na huduma ambapo wafanyabiashara wanapaswa kutoa risiti stahiki kwa wateja wao na wanunuzi wanatakiwa kudai risiti kila wanapofanya manunuzi, wasipofanya hivyo, watawajibika kwa mujibu wa sheria,” alisema Bw. Kayombo.
Mkururgenzi huyo ameongeza kuwa, kitendo cha kutokutoa na kudai risiti kina adhabu zake ambapo mlipakodi asiyetoa risiti, faini yake ni shilingi milioni 1,500,000 hadi 4,500,000 au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja na mnunuzi asiyedai risiti ni adhabu yake ni faini ya shilingi 30,000 hadi shilingi milioni 1,500,000.
“Natoa wito kwa walipakodi na wananchi wote kuhakikisha wanatoa na kudai risiti za EFD ili kuepuka usumbufu na faini ambazo kimsingi zinarudisha nyuma maendeleo ya wahusika watakaokutwa na makosa hayo,” alieleza Bw. Kayombo.
Mkurugenzi huyo wa TRA Bw. Richard Kayombo amewaonya watu watakaojaribu kuharibu kampeni hiyo kwa kujifanya maofisa wa TRA na kueleza kwamba, wakikamatwa watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kutangazwa hadharani.
Amewaomba wananchi wakiwaona watu wa namna hiyo wapige simu bure Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa namba za simu 0800 75 00 75 au 0800 78 00 78 au watume ujumbe kwa njia ya whatsapp 0744 233 333.
Mashine za EFD zilianzishwa mwaka 2010 kwa dhumuni la kuwasaidia walipakodi kutunza kumbukumbu zao za biashara katika mfumo wa kielektroniki ili waweze kukadiriwa kodi stahiki, kuweka uwazi kati ya walipakodi na TRA na kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari.