Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela Mhe Nelson Mesha akizungumza na wanachama waliojitokeza kuadhimisha sherehe za miaka 45 ya Chama hicho
Katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Bi Aziza Isimbula akiwaongoza wanachama katika kufanya usafi wa eneo la ofisi ya Chama hicho
Viongozi mbalimbali wa CCM wilaya ya Ilemela wakikagua jengo jipya la ofisi za Chama hicho lililopo kata ya Buswelu
……………………………………………….
Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ilemela kina mengi ya kujivunia tangu kuzaliwa kwa chama hicho mwaka 1977 ikiwa ni muunganiko wa chama cha TANU na ASP
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ilemela Mhe Nelson Meshack wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 45 tangu kuzaliwa kwa chama hicho zilizofanyika katika viwanja vya jengo la ofisi mpya za wilaya zilizopo kata ya Buswelu ambapo wanachama wake wameshiriki kusaidia shughuli ndogo ndogo za ujenzi wa jengo hilo la ofisi, kufanya usafi, kupanda miti, kujihakiki katika madaftari ya wanachama, kujisajili kielektroniki na kulipa ada za uanachama ambapo mwenyekiti wake amefafanua kuwa wanachama wanapaswa kujivunia uimara wa chama chao, usimamizi wa shughuli za maendeleo, utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi, amani na utulivu uliopo sanjari na kuwaasa kuendelea kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa ambae pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hasan
‘… Kwa neema ya Mungu mwaka huu tumetimiza miaka 45 tukiwa katika mwaka wa uchaguzi wa viongozi kwa ngazi mbalimbali za chama chetu, Upendo umetawala, amani imetawala, Utulivu umetawala, Na tunaamini tutaendelea kuwa wamoja …’ Alisema
Aidha Mwenyekiti Mesha amewafikishia wananchi waliojitokeza katika shughuli hiyo salamu za katibu mkuu wa chama cha mapinduzi Comred Daniel Chongolo aliyewasili mkoa wa Mwanza mapema Januari 31, kuelekea mkoa wa Mara kwaajili ya kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 45 kitaifa huku akiwashukuru wadau mbalimbali waliochangia nguvu na mali katika kukamilisha jengo la ofisi za CCM wilaya
Kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Bi Aziza Isimbula amefafanua kuwa maadhimisho ya sherehe za miaka 45 ya kuzaliwa CCM yamelenga kufanya shughuli za kuimarisha uhai wa chama ikiwemo kuandikisha wanachama wapya, kujisajiri kielektroniki, kulipa ada ya uanachama pamoja na kuimarisha miradi ya kiuchumi kwaajili ya chama
Chama Cha Mapinduzi Ilemela kitahitimisha sherehe hizo kwa ngazi ya wilaya Februari 02, mbali na shughuli nyengine kitakabidhi Saruji za ujenzi wa miundombinu ya elimu ndani ya wilaya ya Ilemela kama ishara ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo