Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) Jaji mstaafu Joseph Warioba akizungumza kabla ya kukabidhi uenyekiti wa Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo Joseph Butiku leo jijini Dar es Salaam
Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere
…………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu
BODI ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), inayomaliza muda wake imemteua Joseph Butiku kuwa mwenyekiti mpya wa bodi hiyo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mwenyekiti wa bodi aliyemaliza muda wake, Jaji mstaafu Joseph Warioba jana wakati akiitambulisha bodi mpya ambayo itakuwa na wajumbe 10.
Warioba alisema bodi iliyomaliza muda wake ambayo ilikuwa inaongozwa na Balozi Dk.Salim Ahmed Salim imefanikiwa kwa kiasi chake hivyo wanaamini kuwa bodi mpya itaendeleza mazuri waliyofanya.
Alisema Hayati Mwalimu Julius Nyerere alianzisha taasisi hiyo mwaka 1996 ikiwa haina fedha ila walijitahidi kusuluhisha migogoro ya ndani na nje ambapo moja ya mgogoro waliofanikiwa ni wa Burundi.
Alisema wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali ila wanashukuru wameweza kuzivuka.
“Tangu mwaka 1996 tumekuwa tukishiriki kwenye mazungumzo ya maridhiano ambapo mengi ya mazungumzo yameweza kufanikiwa ni imani yetu kuwa bodi mpya ambayo ina wajumbe wa zamani wawili itaendeleza utaratibu huo kwa maslahi ya Tanzania na Afrika kwa ujumla,” alisema.
Warioba alitoa rai kwa Watanzania kuiunga mkono bodi hiyo mpya ili iweze kutimiza malengo hayo ambayo mwasisi wake Hayati Nyerere aliyasisi.
Kaimu Mwenyekiti huyo, alitaja wajumbe wapya wa bodi ni Profesa Tarsis Kabwegijere, Balozi Amina Salum Ally, Neema Nyerere, Geoffrey Israel, Catherine Mgenda, John Kyaruzi, Balozi Celestine Liundi, Profesa Penina Mlama na Profesa Martha Koro.
Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Butiku alisema mipango yake ni kuhakikisha dhana ya amani, umoja na maendeleo kwa kasi ambayo italeta mabadiliko chanya kwa wananchi na nchi
Butiku ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MNF alisema katika uongozi wake atahakikisha kasi ya kudumisha umoja, mshikamano na maendeleo inafanikiwa.
“Mimi nipo kwenye hii taasisi tangu 1996 malengo na matarajio yake nayajua na nimekuwa nikiyatekeleza naamini nafasi hii itanipa nguvu zaidi kusukuma mbele zaidi,” alisema.
Butiku alisema taasisi hiyo itahakikisha malalamiko yote ya kisiasa, kijamii, uchumi na maendeleo yanapata muafaka kwa njia shirikishi kwani ndio lengo la Hayati Nyerere.