Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akihutubia mkutano wa 15 wa mwaka wa Chama cha Wadau wa Mazao yenye Thamani Kubwa ambayo ni mboga, matunda na viungo (TAHA) mapema leo katika ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha.
Mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongella akitoa neno kwa Washiriki wa mkutano wa 15 wa mwaka wa Chama cha Wadau wa Mazao yenye Thamani Kubwa ambayo ni mboga, matunda na viungo (TAHA) mapema leo katika ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha.
Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo naye alishiriki kwenye mkutano huo wa 15 wa mwaka wa Chama cha Wadau wa Mazao yenye Thamani Kubwa ambayo ni mboga, matunda na viungo (TAHA) mapema leo katika ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha.
************************
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe leo tarehe 29 Januari, 2022 ametangaza rasmi kurejea kwa Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu kama Nane Nane kwa mwaka 2022.
Waziri Bashe ametangaza rasmi uamuzi huo wakati akifungua mkutano wa 15 wa mwaka wa Chama cha Wadau wa Mazao yenye Thamani Kubwa ambayo ni mboga, matunda na viungo (TAHA) katika Hoteli ya Mount Meru ya Jijini Arusha.
Waziri Bashe amesema baada ya timu ya Wizara kupitia na kubuni namna bora ya kuendesha maonesho kulingana na mazingira ya sasa; Maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) yatakuwa ya tofauti ukilinganisha ya miaka kadhaa iliyopita.
Waziri Bashe amesema jambo la kwanza ambalo limeboreshwa ni uendeshaji wa maonesho hayo ili yawe endelevu; Ambapo Wizara kwa kushirikiana na Secretarieti za mikoa ni kuanzisha Vituo vya mafunzo kwa Wakulima msimu wote wa mwaka na wakati huo Vituo hivyo kuwa atamizi (Incubate) kwa Wakulima kwa kutumia teknolojia mbalimbali za kilimo katika kipindi chote cha mwaka.
Jambo lingine alilolitaja Waziri Bashe ni Vituo hivyo kuendelea kutoa mafunzo kwa Wakulima kwa kipindi cha mwaka mzima na wakati huo huo kuwa sehemu ya kuzalisha mazao ya kilimo kwa kuwa sehemu zote za maonesho zina mashamba madogo na makubwa.
Waziri Bashe ameongeza kuwa hivi karibu Wizara kwa kushirikiana na Serikali za mikoa zitautangaza mkoa mwenyeji wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nane Nane kwa mwaka 2022.
Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) kwa mwaka 2021 hayakufanyika; Yalihairishwa kwa tangazo la Waziri wa Kilimo wa wakati huo Prof. Adolf Mkenda. Tangazo alilolitoa tarehe 10 Februari, 2021 Jijini Dodoma ambapo ilielezwa kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Secretarieti za mikoa zinafanya tathmini ya namna bora ya kuyaendesha maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) kwa namna bora.
Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi (Nane Nane) yalianza rasmi Mwezi Agosti mwaka 1994 na yamekuwa yakiadhimishwa Kitaifa kwenye Kanda Nane (8) kama ifuatavyo: – Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, uwanja vya John Mwakangale, Uyole, Jjijini Mbeya; Kanda ya Kaskazini, uwanja wa Themi, Jijini Arusha; Kanda ya Mashariki, uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Manispaa ya Morogoro; Kanda ya Ziwa, uwanja wa Nyamhongolo, Jijini Mwanza; Kanda ya Kati, Uwanja wa Nzuguni katika Jiji la Dodoma; Kanda ya Magharibi, Mkoani Tabora katika uwanja wa Ipuli; Kanda ya Ziwa Mashariki, Mkoa wa Simiyu katika uwanja wa Nyakabindi na mwisho ni Kanda ya Kusini, Mkoani Lindi katika uwanja vya Ngongo.