Kamishna Msaidizi Idara ya Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Tullo Msanja akizungumza katika kikao cha robo mwaka wadau wa masuala ya Ustawi wa Jamii katika utekelezaji wa afua mbalimbali za utoaji wa huduma za Ustawi wa Jamii nchini kilichofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya wadau kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wizara, Taasisi za Serikali na Shirika la Pact Tanzania wakiwa katika kikao cha robo mwaka wadau wa masuala ya Ustawi wa Jamii katika utekelezaji wa afua mbalimbali za utoaji wa huduma za Ustawi wa Jamii nchini kilichofanyika jijini Dodoma.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM
………………………………………………………….
Na WMJJWM Dodoma
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imekutana na wadau wa masuala ya Ustawi wa Jamii nchini kujadili utekelezaji wa afua mbalimbali za utoaji wa huduma za Ustawi wa Jamii nchini ili Afua hizo ziwe na tija kwa Jamii inayo hudumiwa.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara jijini Dodoma Kamishna Msaidizi Idara ya Ustawi wa Jamii, Tullo Msanja amesema, Wizara inashirikiana na wadau ili kuhakikisha huduma za ustawi wa jamii nchini zinaboreshwa na Maafisa Ustawi wa Jamii wanatumika ipasavyo ziweze kufanikisha huduma hizo.
Ameongeza kuwa, kuna haja ya kuimarisha ushirkiano wa kada zinazohusika na utoaji wa huduma kwa jamii ziweze kusaidia kupunguza changamoto za upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii ili na kufanya huduma za Ustawi wa Jamii ziendelee kutolewa kwa jamii hadi katika ngazi za mtaa/ kijiji.
“Wizara itaendelea kuratibu vikao vya wadau vya kila robo mwaka na kuhakikisha wadau wanatoa taarifa za utekelezaji katika utoaji wa huduma za ustawi wa jamii nchini” amesema Masanja.
Akizungumza kwa niaba ya wadau, Mwakilishi wa Shirika la Pact Tanzania Elias Hackee amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa, mifumo iliyowekwa ya utoaji wa huduma za Ustawi wa Jamii inaimarishwa kuwezesha huduma hizo zitolewe kwa ufanisi na kuwafikia walengwa kwa wakati muafaka.
“Mifumo ikikaa vizuri hata matumizi ya rasimlai zilizopo hususani fedha utaratibiwa vizuri na kufanikisha yale yaliyokusudiwa ya kutoa huduma za ustawi wa jamii kwa makundi yenye uhitaji wa huduma hizo” alisema Bw. Elias