……………………………………………………..
NA FARIDA SAID.MOROGORO
Shule ya msingi Mchikichini iliyopo Manispaa ya Morogoro inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati zaidi ya 200 hali inayowalazimu Wanafunzi 171 wa darasa la saba kukaa kwenye chumba kimoja cha darasa.
Hayo yameelezwa na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Mtindo Ismail wakati wa kupokea mifuko 70 ya saruji iliyotolewa na baadhi ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka 2001katika shule hiyo.
Mwalimu Ismail amesema shule hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa ambapo kwa sasa shule inamadarasa 7 huku upungufu ukiwa ni madarasa 20, hali inayowalazimu wanafunzi kukaa kwa mlundikano katika vyumba vya madarasa.
“Kwa mfano darasa la saba wa sasa wapo 171 na wote wanakaa katika darasa moja, kiuhalisia walitakiwa wawe katika mikondo mitatu na madarasa matatu kutoka na uhaba wa madarasa wote hawa wanakaa katika chumba kimoja.” Alisema mwalim Mkuu.
Pamoja na uhaba wa vyumba vya madarasa shule hiyo pia inakabiliwa na upungufu wa madawati, ambapo Mwalimu Mkuu amesema kuna wanafunzi ambao wanakosa madawati na kulazimika kukaa chini.
Amesema upungufu wa madawati unatokana na hamasa kubwa walioipata wazazi ya kuwaandisha Watoto wao darasa la kwanza ambapo mpaka sasa Watoto 146 wameandikishwa shuleni hapo.
Kutokana na changamoto hizo umoja wa wanafunzi waliosoma shule ya Msingi Mchikichini wakiongozwa na Mweyekiti wao Wakili Msomi Johnson Kakiziba wamesema watashirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zilizopo shuleni hapo sambamba na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kutatua changamoto hizo.
Wanafunzi hao waliomaliza Mwaka 2001 Shule ya Msingi Mchikichini wametoa mifuko 70 ya saruji, mikebe, kalamu pamoja na rula kwa wanafunzi wote wa darasa la saba wa mwaka huu katika shule hiyo kama sehemu ya shukrani zao na kukumbuka walipotoka.
Kwa upande wao wanafunzi wa darasa la saba shuleni hapo waliopata fulsa ya kupata zawadi ya kalamu, mkebe pamoja na rula kwa niaba ya wengine wakatoa shukulani zao na kutoa ahadi kwa kaka na dada zao kuwa watasoma kwa bidii na kupata matokeo mazuri katika mtihani wao wa darasa la saba.