…………………………………………………..
Na John Walter-Babati
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Babati mkoani Manyara Abdulrahman Kololi, amewataka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mjini hapo kujijengea utaratibu wa kutoa taarifa kwa madiwani kuhusu miradi wanayotekeleza katika maeneo yao.
Ametoa wito huo kwenye Baraza maalum Halmashauri ya mji wa Babati ambalo lililenga kutoa maoni na ushauri katika Mapendekezo ya mpango wa bajeti wa matengenezo ya barabara wa TARURA Halmashauri ya mji wa Babati kwa mwaka 2022-2023.
Mheshimiwa Kololi amesema ushirikishwaji unaondoa malalamiko kwa Viongozi wa eneo husika na kuongeza ufanisi wa kazi.
Aidha amesema kilomita moja ya barabara ya lami Katika kijiji cha Nakwa ni fedha za Mfuko wa Jimbo kama alivyoahidi Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini Paulina Gekul.
Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) Katika Mwaka wa fedha 2022/2023 katika Halmashauri ya mji wa Babati imeomba kutengewa bajeti ya Shilingi Milioni 763,710,000.00 bajeti ya ukomo na bajeti isiyo ya ukomo ni kiasi cha shilingi 9,782,007,500.00.
Kwa mujibu wa Meneja wa TARURA Mji wa Babati Mhandisi Selemani Mzirai, bajeti hiyo ni kwa ajili ya matengenezo ya barabara,madaraja na ujenzi wa mifereji.
Mzirai amesema fedha ya tozo iliyotolewa na serikali shilingi Milioni 500 zitaelekezwa kwenye kata zote nane na Milioni 500 za mfuko wa Jimbo zimeelekezwa kujenga kwa kiwango cha Lami barabara ya kijiji cha Nakwa.
Diwani wa kata ya Mutuka Yona Wawo amesema hali ya barabara ya Mutuka ni mbaya na endapo haitarekebishwa itaua watu kwa ajali,”naomba nirudie tena hali ni mbaya sana na isiporekebishwa itaua” alisisitiza Mheshimiwa Yona.
Diwani wa kata ya Bonga Hiiti Mutlo ameishauri TARURA ijenge Barabara zote za mji wa Babati kwa kiwango cha Changarawe ili barabara zote zirekebishwe kwa kuwa gharama inakuwa ndogo tofauti na kuweka lami barabara chache kwa gharama kubwa, ambao umeungwa mkono na madiwani wengi walioshiriki katika baraza hilo maalum.
Kwa Upande wake diwani wa kata ya Babati Haroun Msalu amesema hata kama madiwani wenzake wanataka Changarawe katika kata zao yeye anataka Lami.
Katibu tawala wilaya ya Babati Khalifan Matipula amesema hatua ya kuwapa nafasi madiwani ni nzuri huku akiitaka TARURA kuyafanyia kazi ushauri uliotolewa.
Daniel Muhina Katibu CCM Babati Mjini amewapongeza TARURA kwa kutii takwa la serikali la kuwashirikisha madiwani kwenye mpoango wa bajeti ili waweze kutoa maoni.
Uamuzi huo wa TARURA kukutana na Madiwani unafuatia baada ya malalamiko ya kuwa maamuzi ya barabara ipi ijengwe yamekuwa yakifanywa na Wataalamu wa TARURA katika ngazi ya mkoa,badala ya uamuzi huo ufanywe katika ngazi ya halmashauri.