…………………………………………………..
Adeladius Makwega,DODOMA.
Kabila la Wajita linatapatikana katika mkoa unaofahamika kama Mara, uliopo kandokando ya upande mmojawapo wa Ziwa Victoria. Jina lao la asili siyo WAJITA bali ni BAJITA ambapo BAJITA inajumuisha watu wate wanaozungumza KIJITA.
Asili ya kabila hilo inaanza mwaka 1890 wakati wa ujio wa Wajerumani kandokando ya Ziwa Victoria kulikuwa na mlima unaofahamika kama MASITA, Wajerumani walipouliza jina la mlima huo walijibiwa kuwa unaitwa MASITA na hapo ndipo wale waliokuwa wakiishi jirani na milima huo wakajulikana kama BAJITA.
Inaaminika kuwa kabila la Wajita wanazo koo kubwa tano nazo ni Wabalinga, Wabaganda, Wabatimba, Wabagunda, na Wabakome. Ikiaminika kuwa kabla ya ujio wa wakoloni koo hizi kila moja iliisha katika eneo lake.
Ili msomaji wangu uweze kulifahamu vizuri kabila la Wajita leo nitajaribu kuelezea asili ya kila koo hizo tano nahakika msomaji wangu utakuwa na nafasi nzuri ya kuwafahamu ndugu zetu hawa.
Ukoo wa Wabalinga iliaminika kuwa ulitokea Bukoba na kufika Mara kwa boti kando kando ya visiwa vya Ukerewe katika eneo linalofahamika kama Kamasi na watoto wanne wa ukoo huo walifika huko Basigu kazi yao kubwa ikiwa ni uvuvi na ufuaji wa vyuma.
Ukoo wa Wabatimba unaaminika huu ulitokea huko Morogoro kwa Wakaguru, Waluguru na Wapogoro. Hawa walifika huku kwa nia moja ya uwindaji tu kwa njia ambayo baadaye ilikuwa ni njia ya reli ya kati. Ndugu zangu hawa waliweka kambi Butimba ambalo eneo hilo baadaye kikajengwa Chuo cha Ualimu Butimba.
Wakaenda Ushashi na wakaweka makazi huko Nyang’ombe wakatengeneza mji uliokuwa unafahamika kama Kagulu. Baada ya muda wakaenda eneo linalofahamika kama Bwasi ambalo wapo hadi sasa.
Eneo hilo la Bwasi lilikuwa na waakazi wa asili ambao ni Baija. Batimba waliwafurusha hawa jamaa katika makaazi hayo na kuishi wao. Uwezo huo wa kuwafurusha wenyeji ulitokana na wao kuwa na ujuzi mkubwa wa kupigana na kuwinda kwani walikuwa na silaha na walikuwa wametoka mbali mno hadi kufika huko.
Shida ilitokea baada ya binti mmoja wa Wabatimba aliolewa na na Mbaija ambapo mtoto aliyezaliwa alikuwa na wajibu wa kutawala eneo la Wabaija. Wabatimba wakagoma na hapo mgogoro kuanza na ndipo kukawa na kufukuzana huko.
Wabatimba ni ukoo wa watawala na hata walipokuja wakoloni, wao waliwapokea vizuri na jambo hili liliwafanya wao kuaminika na mwisho wa siku waliendelea kuwa watawala wa koo zingine za Wajita. Kumbuka kusafiri kutokea Morogoro hadi Ujitani ni mwendo mrefu huko njiani walijifunza mengi na ndiyo maana hata mzungu aliwakubali kwa haraka kuliko koo zingine za Wajita.
Ndiyo maana waswahili wanasema mkaa bure si mtembea bure huenda akaokota.
Ukoo wa tatu wa Wajita ni Wabakome, ikiaminika kuwa kwa asili wanatokea huko Bukoba katika eneo linalofahamika kama Iyangillo. Pia wapo akina Bakome wa Uzinza, Uzanaki, na makabila mengine ya Uganda. Hawa akina Bakome wanaishi katika eneo linalofahamika kama Butimba.
Ukoo wanne ni Wabagamba, hawa wanapatikana huko Nyang’ulukulu kusini mwa Butimba wakitokea huko Legamba, eneo la Ushashi. Kazi yao kubwa ilikuwa ni uwindaji wa Viboko.
Ukoo wa tano ni Wabagunda, ukoo huu unatokana na neno la kijita KUGUNDA ikimanisha kuwinda. Wakitokea eneo la Uzanaki kwa Chifu Manyali na wakaweka makazi hapo Bugonja wakiwinda tembo na na nyumbu.
Msomaji wangu kwa leo naishia hapo usikose matini ijayo ambapo nitaendelea kulitazama kabila hili kwa kina hususani utani wake na Wabaluguru. Nakutakia siku njema.
0717649257