…………………………………..
Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Prof. Dos Santos Silayo amewasili wilayani Magu mkoni Mwanza tayari kwa ziara ya kikazi ya siku moja katika hifadhi ya Msitu wa Sayaka. Kamishna wa Uhifadhi ambaye amesafiri kwa njia ya barabara akitokea jijini Dodoma ambapo napo alikuwa na ziara yenye lengo la kuhakikisha na kukagua shughuli za usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki sambamba na kuona namna gani Wakala kupitia ofisi zake za Kanda, Wilaya na mashamba zinaendelea kuboresha uwezo wa kutoa huduma kwa umma.
Mara baada ya kuwasili mkoani Mwanza Kamishna wa Uhifadhi alitembelea kituo Ofisi ya Mhifadhi wa Wilaya TFS wilani Magu na kupata nafasi ya kuzungumza na watendaji wake. “Niwapongeze kwa kazi kubwa mnayofanya kuhakikisha mnahifadhi vyanzo vya maji vya mito miwili ya Duma na Simiyu vilivyopo kwenye Msitu wa Sayaka, na kutiririsha maji yake kuelekea Ziwa Viktoria,”alisema Kamishna wa Uhifadhi.
Aidha aliwaambia watendaji hao kuendelea kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Magu inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Salum Kali ili kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki wilani Magu huku rasilimali hizo zikichangia kikamilifu mahitaji ya kijamii, kiuchumi, kiikolojia na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi – TFS, Kamanda wa Kanda ya Ziwa Mohamed Bakari amesema licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za mawasiliano baina ya sekta moja na nyingine, za kisheria ama utendaji wa kawaida katika usimamizi wa rasilimali misitu na nyuki, TFS kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya umekuwa ukitumia fursa zote zinazopatikana kwenye uhifadhi kukuza kipato cha wananchi wanaoizunguka misitu ya hifadhi.
Aidha, Kamishna wa Uhifadhi – TFS alipata bahati ya kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Salum Kali ambapo pamoja na mambo mengine alimpongeza kwa kazi kubwa inayofanywa Wakala katika kuhakikisha inapanua wigo wake kibiashara na kuongeza maeneo ya uzalishaji miti na mazao ya nyuki ili kukidhi mahitaji halisi, kufungua milango katika shughuli za uwekezaji, kuboresha njia mbadala za mapato kama vile kuja na zao la utalii ikolojia na uboreshaji wa hifadhi za misitu na nyuki kwa ujumla.