***************
SINGIDA: Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi inatarajiwa kukabidhi misitu mitatu kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ili kuepukana na migongano ya kiutendaji na usimamizi unaosababisha kulegalega kwa utekelezaji wa sheria katika uhifadhi.
Akizungumza katika kikao kifupi ofisini kwake na Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo jana, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Jerry Muro alisema wamefikia uamuzi wa kutoa miliki ya misitu hiyo kwa TFS ili kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020 -2025) inayoagiza kuanzishwa kwa mamlaka moja ya misitu na nyuki nchini.
Muro alisema mojawapo wa changamoto anayokumbana nayo hivi sasa ni uharibifu mkubwa wa misitu katika msitu wa Minyunge, Mlilii na Wembere unaosababishwa na wavunaji haramu wa miti kwa ajili ya mkaa unaopelekwa Singida mjini.
“Asilimia 80 ya mkaa wote wa Mkoa wa Singida unatoka kwenye misitu hii. Kwangu magunia mamia kwa mamia yanasafirishwa usiku na punda kwenda mjini kinyume na taratibu, sasa tukasema tuwapeni misitu hii TFS halafu sasa nyinyi mkiamua kuweka doria na kuanza kuchukua hatua tuwe kwenye mikono salama,” alisema Muro.
“Halmashauri zetu hazina resource (rasilimali) za kutosha, lakini pia watendaji hakuna. Utakuta halmashauri ina ofisa mazingira mmoja tu ambaye kwa kweli anazidiwa na hawezi kupambana na mambo makubwa ya misitu hii. Hivyo tunakwenda kukupa misitu hii ili sasa twende kwenye uhifadhi endelevu na kuhakikisha mnaratibu na kusimamia misitu hii tukiamini mtatukumbuka kwenye mapato yatakayokwenda kupatikana kupitia uhifadhi.”
Akizungumzia zaidi kuhusu mchakato wa umilikishwaji wa misitu hiyo, Muro alisema hatua zote za kuitoa misitu hiyo zimefuata sheria, kanuni na taratibu na tayari zimeshakamilika huku kilichosalia ni kufanya hafla ya makabidhiano.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Silayo alimpongeza Muro kuanzisha mchakato huo kwa kushirikisha pande zote katika mijadala baada ya kutembelea na kuona hali halisi ya misitu na kuahidi kuwa watahakikisha wananchi wanaozunguka misitu hiyo wananufaika moja kwa moja na hatua hiyo ya kuikabidhi kwa TFS.
“Tunaamini uamuzi huu utakwenda kutusaidia kuwa na mamlaka ya kudhibiti misitu hii, kwani sasa hakutakuwa na changamoto ya mawasiliano baina ya sekta moja na nyingine, iwe ya kisheria ama utendaji wa kawaida katika usimamizi wake. Lakini tunakwenda kutumia fursa zote zinazopatikana kwenye uhifadhi kukuza kipato cha wananchi wa Singida,” alisema Profesa Silayo.
Kamishna huyo alisema licha ya changamoto ya mkinzano wa kisekta katika maeneo mengine ya nchi, TFS itaendelea kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki ili kuchangia kikamilifu mahitaji ya kijamii, kiuchumi, kiikolojia na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho.