Na Dotto Mwaibale, Singida.
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Alhajj Juma Killimbah ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa wilayani humo.
Kilimba ametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya jana ya kukagua miradi hiyo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kufanya mikutano na wananchi ilikujua changamoto walizonazo na kuzitafutia utatuzi.
Kilimba alitoa pongezi hizo baada ya kuridhishwa na utekelezwaji wa ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Msingi Msange ambayo yalikuwa katika hali mbaya na kushindwa kutumika kutokana na uchakavu.
“Nilifika hapa miezi mitatu iliyopita nikiwa na wajumbe wa kamati ya siasa mkoa ambapo madarasa haya tuliyakuta yakiwa katika hali mbaya ndipo nilipotoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanatafuta fedha kwa ajili ya kuyakarabati na mshukuru sana mkurugenzi huyo kwa kutekeleza agizo hilo baada ya kutoa fedha Sh. 17,500,000 kutoka mapato ya ndani na kukamilisha ujenzi huo” alisema Killimbah.
Akizungumza wakati akiendelea kukagua miradi aliipongeza wilaya hiyo kwa kuitendea haki miradi ambayo Serikali imetumia fedha nyingi kuitekeleza hasa ujenzi wa madarasa yaliotokana kwa fedha za mradi wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid-19.
Kilimba alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwan kutoa fedha hizo na kuwaomba viongozi ilipo miradi hiyo kuwahamasisha wananchi wao kuitunza.
Alisema Serikali inafanya kazi kubwa ya kutoa fedha za miradi na ni wajibu wa wananchi nao kuhamasika kuunga jitihada za serikali kwa kujitolea kufanya kazi zingine za maendeleo ambazo zipo ndani ya uwezo wao.
Killimbah alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa madarasa hayo ambayo kwa mkoa mzima zimetumika Sh.13.4 kumewaondolea adha ya kusoma katika mazingira yasiyo rafiki kwa wanafunzi kuanzia shule shikizi, msingi na sekondari.
Alisema hivi sasa nchini kote baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya kazi kubwa ya kutoa fedha hizo wananchi hawazungumzii tena ujenzi wa madarasa au ukosefu wa madawati kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Aidha Killimbah alisema mwaka huu kutakuwa na uchaguzi wa ndani wa viongozi watakaoshika nafasi mbalimbali kuanzia ngazi ya mashina, vitongoji, kata, wilaya hadi mkoa ambapo aliwaomba Wana CCM wote kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini Ramadhani Ighondo alimpongeza Kilimbah kwa ufuatiliaji wa ahadi yake kama alivyoahidi kurudi kuyagua tena madarasa ya shule hiyo ya Msange na kuwa kazi hizo za maendeleo zinazofanyika ni utekelezaji wa ilani ya CCM na kuwa wataendelea kufanya hivyo.
“Tutaendelea kuwatumikia wananchi kwa kufanya kazi za maendeleo na nichukue nafasi hii kumshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali” alisema Ighondo.
Katibu wa CCM Mkoa wa Singida Idara ya Oganaizesheni Dafroza Lucas akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Jangwa katika ziara hiyo aliwahimiza wakati wa zoezi la Sensa ya watu na makazi litakapo wadia mapema mwaka huu wajitokeze kwa wingi kuhesabiwa.
Baadhi ya miradi iliyokaguliwa na Mwenyekiti huyo wa CCM ambaye aliambatana na kamati ya utekelezaji ya wilaya hiyo ni mradi wa ujenzi wa madarasa mawili Shule ya Msingi Msange, kukagua kukamilika kwa madarasa ya Uviko Shule ya Sekondari ya Madasenga iliyopo Kijiji cha Mangida na Shule ya Msingi ya Jangwa ambayo inachangamoto kubwa ya kutokuwa na vyoo.
Killimbah katika ziara hiyo alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi wa Vijiji vya Mangida, Sefunga na Hendeshi ili kujua changamoto zao ziweze kutafutiwa ufumbuzi.
Katika hatua nyingine kabla ya kuanza kwa ziara hiyo Killimbah pamoja na wajumbe wa kamati hiyo ya utekelezaji ya wilaya hiyo walikwenda kutoa rambirambi nyumbani kwa Mzee maarufu wa Ilongero na muasisi wa CCM, Seif Muhomi ambaye alifariki usiku wa kuamkia jana.