***************************
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imekuwa ikifuatilia vitendo vya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kusababisha mauaji ya kikatili katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Katika ufuatiliaji wake THBUB imebaini yafuatayo:
- Kumejengeka tabia ya baadhi ya wananchi kutokuzingatia sheria za nchi na kujichukulia sheria mikononi;
- Vitendo vya mauaji vilivyotokea mfululizo hivi karibuni vimeambatana na ukatili dhidi ya ubinadamu;
- Katika baadhi ya mauaji yaliyotokea kuna viashiria vya ulipaji kisasi;
- Katika baadhi ya mauaji kuna viashiria vya imani za kishirikina;
- Baadhi ya wananchi wanajenga dhana kuwa wanaweza kutenda uovu wasiweze kukamatwa;
- Kuna viashiria vya wananchi kutokuwa na imani na vyombo vya usimamizi wa haki; na
- Baadhi ya wananchi wasiopenda kufanya kazi halali kuwa na tamaa ya mali.
THBUB inatamka kuwa vitendo vya mauaji vilivyotokea hivi karibuni ni:
- Ukiukwaji wa haki ya kuishi kama ilivyotamkwa katika Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na hivyo inalaani vikali vitendo hivyo;
- Ukatili dhidi ya binadamu ambao ni kinyume na Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; na
- Baadhi ya wananchi kutoheshimu Katiba na Sheria za nchi kinyume na Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri na Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inatambua jitihada na maelekezo yaliyotolewa na viongozi wa Serikali hivi karibuni katika kukomesha mauaji ya raia nchini. Pamoja na hayo, Tume inapendekeza yafuatayo:
- Jeshi la Polisi
- Lichukue hatua mahsusi kuimarisha ulinzi katika maeneo ya wananchi na kuwezesha kupata taarifa za mapema kuhusu kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa sheria ikiwa ni pamoja na mauaji na vitendo vya ukatili, kabla na baada ya matukio hayo kutokea kwa kushirikiana na wananchi katika maeneo husika ili kusaidia ulinzi na usalama wa raia; na
- Kwa matukio yaliyoripotiwa, Jeshi la Polisi lihakikishe watu wote waliohusika na mauaji hayo wanakamatwa ili sheria ichukue mkondo wake.
- Serikali za Mitaa
Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ngazi zote ziwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha kunakuwepo taratibu za kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yao.
- Viongozi wa Dini
Waongeze nguvu katika utoaji wa elimu ya dini na maadili na kukemea uovu unaotokea nchini.
- Wananchi
- Wajenge utamaduni wa kuheshimu sheria za nchi na haki za binadamu;
- Watafute namna bora ya kupata suluhu ya migogoro inayowakabili katika ngazi zote za jamii kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa badala ya kujichukulia sheria mkononi;
- Washirikiane na vyombo vya dola kufichua maovu na kubaini uvunjifu wowote wa sheria na haki za binadamu ndani ya jamii, na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuzuia matukio kama hayo kutokea, au kusaidia katika upelelezi wa mauaji na matendo mengine ya uvunjifu wa sheria yaliyotokea; na
- Kwa wananchi hasa waishio vijijini waendeleze utamaduni wa kujuliana hali wanapoamka asubuhi.
- Asasi za Kiraia na Vyombo vya Habari
Asasi za Kiraia, Vyombo vya Habari na wadau wengine waendelee kutoa elimu kwa umma kuhusu taratibu zilizopo za namna ya kushughulikia masuala mbalimbali ya kijamii kupitia sheria na hivyo kulinda haki za binadamu na utu wa mtu.
Tume itaendelea kutoa ushirikiano katika jitihada za kukomesha mauaji ya raia kwa kuelimisha umma kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Mwisho, Tume inatoa pole kwa ndugu, jamaa na wanafamilia waliopoteza wapendwa wao katika matukio haya na kwa waliopatikana na majeruhi.
Jukumu la ulinzi na utetezi wa haki za binadamu ni letu sote!