Na Mwandishi Wetu, Singida
WAWEKEZAJI mkoani Singida
wametakiwa kushirikiana na Halmashauri za wilaya wakati wa kuanzisha
miradi ya Maendeleo ya Kijamii
(Community socially responsibility – CSR ) ili kukubaliana aina za miradi
na namna itakavyotekelezwa lengo likiwa ni kuepuka matumizi makubwa ya
fedha kwa kazi ambazo zingetumia fedha kidogo.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa
Mkoa huo Dk. Binilith Mahenge leo January 26, 2022 alipotembelea machimbo
ya madini ya dhahabu yanayochimbwa na Kampuni ya Shanta Gold iliyopo
Kijiji cha Mang’onyi wilayani Ikungi ambapo alieleza kwamba miradi yote
inayoanzishwa na wawekezaji ipitie katika Halmashauri za wilaya ambazo
zinafahamu mahitaji ya wahusika na gharama halisi za ujenzi katika
maeneo hayo.
Akitolea mfano kwa madarasa
yaliyokamilika hivi karibuni kupitia fedha za uviko 19 Mahenge alisema
kila darasa liligharimu kiasi cha Sh.milioni 20, ikilinganishwa na madarasa
yaliyojengwa na Shanta Gold ambayo yamegharimu Sh.milioni 28 kwa kila
darasa.
“Kama mradi huu mgeshirikisha
Halmashauri kwa kiasi kikubwa mngetumia Force Account na mngepata wakandarasi
wa bei ndogo na fedha zingebaki zikafanya maendeleo mengine katika jamii.
Niwashauri mshirikiane ipasavyo na Halmashauri kupanga aina ya miradi
mnayotaka kuipeleka kwa jamii”, alisema Mahenge.
Hata hivyo Mahenge ameipongeza
kampuni hiyo ya Shanta Gold kwa kutumia zaidi ya milioni 190 kwa kupeleka
huduma kwa jamii ikiwemo ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na uchimbaji wa
visima vya maji huduma ambazo zinafaidisha vijiji vya Mang’onyi, Sambaru,
Mlumbi, Tupendane na Mwau.
Aidha, Dkt. Mahenge ameitaka jamii
inayozunguka mgodi huo kutumia fursa na kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi
mbalimbali ikiwemo ufugaji wa kuku na mama lishe pamoja na kuomba ajira
katika kampuni hiyo kwa kuwa kadri mradi unavyokuwa ndivyo mahitaji
yatakavyoongezeka.
Awali akitoa taairifa ya mgodi
Meneja wa mradi huo Kundael Mtiro alisema mpaka kufikia sasa mradi ulitakiwa
kufikia asilimia 46.14 katika utekelezaji wake lakini kwa sababu ambazo
zimekuwa nje ya uwezo mpaka sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia
43.62 .
Hata hivyo Mtiro akaendelea
kufafanua kwamba mpaka Juni,2022 mradi utakuwa unakamilisha robo ya nne
ya mwaka ambapo wanategemea kwamba utakuwa umekamilika kwa kuwa tayari
washasimika mabomba katika maeno yote yanayohusika pamoja na uchimbaji wa
visima, ujenzi wa ofisi na makazi umekamilika kwa asiliami 80.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Murro
alisema mgodi huo utainua uchumi wa Singida na taifa kwa ujumla ambapo
utasisimua sekta nyingine za elimu barabara, zahanati na wananchi kupata ajira.
Alisema wilaya imeendelea kusimamia
hali ya usalama katika eneo la mradi na imehakikisha wanachi wote
waliokuwa wanastahili kupata fidia zao wamelipwa kwa wakati.