Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Mkutano wa Dunia wa kusherehekea Mafanikio ya Miaka 10 ya Tamko la London na Kuzindua Tamko la Kigali uliofanyika kwa njia ya Mtandao, Ikulu Chamwino Mkoani leo tarehe 27 Januari, 2022.
*********************************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 27 Januari, 2022 ameshiriki kwa njia ya mtandao Mkutano wa Dunia wa kusherehekea mafanikio ya miaka 10 ya Tamko la London na kuzindua Tamko la Kigali la kujitoa kwa asilimia 100 kutokomeza Magonjwa ya Tropiki Yasiyopewa Kipaumbele (NTDs).
Katika Mkutano huo, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania ni moja ya nchi zilizoathirika kwa kiasi kikubwa na magonjwa hayo ambapo zaidi ya watu milioni 29 duniani wanahitaji matibabu ya angalau ugonjwa mmojawapo.
Mhe. Rais Samia amesema magonjwa hayo hasa minyoo ya tumbo kwa watoto huathiri makuzi ya akili na huwafanya kukosa fursa ya kupata elimu kwa wakati sahihi.
Mhe. Rais Samia amesema kupambana na magonjwa hayo kunahitaji uwekezaji mkubwa ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma na ufuatiliaji wa kutosha.
Aidha, Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa uchache wa rasilimali na vipaumbele shindani vimekuwa vikizuia jitahada za kupunguza na kutokomeza kasi ya ueneaji wa magonjwa hayo.
Vile vile, Mhe. Rais Samia amesema licha ya changamoto zinazojitokeza, Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele kutokana na mikakati madhubuti ya Serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
Pia, Mhe. Rais Samia ametolea mfano Tanzania kwa baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika kupambana na magonjwa hayo kwa baadhi ya Wilaya ambapo maeneo husika yaliyohitaji matibabu ya kinga dhidi ya ugonjwa wa matende imepungua kutoka wilaya 119 mwaka 2004 hadi kufikia wilaya 8 mwaka 2021.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania imepunguza idadi ya wilaya zinazohitaji matibabu ya kuzuia Trakoma kutoka wilaya 71 mwaka 2012 hadi kufikia wilaya 9 mwaka 2021, na pia imepunguza idadi ya watu wanaohitaji upasuaji wa Trakoma kutoka 167,000 mwaka 2012 hadi 27,000 Desemba 2021.
Mhe. Rais Samia amesema anaamini kwamba, kupitia mkutano huo, maisha ya wananchi yatabadilika ikiwemo mamilioni ya wasichana na wanawake nchini Tanzania ambao wapo katika hatari ya kuambukizwa magonjwa hayo.
Pia Mhe Rais Samia amebainisha kuwa dhamira walioahidi katika mkutano huo itasaidia kujenga usawa wa upatikanaji wa huduma bora za afya, ambayo ni muhimu katika kupunguza maambukizi ya magonjwa hayo yanayoweza kuzuilika.
Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia amesaini Azimio la Kigali kuhusu Magonjwa ya Tropiki Yasiyopewa Kipaumbele (NTDs) ili kujitoa kwa asilimia 100 kutekeleza Azimio hilo.