*************************
Na John Walter-Hanang
Kituo cha Afya cha Mogitu kilichopo kata ya Mogitu wilayani Hanang Mkoani Manyara kimeanza kufanya kazi ikiwa ni siku chache baada ya waziri mkuu kufika katika kituo hicho na kutoa agizo Wananchi waanze kupatiwa huduma kituoni hapo ili kuwapunguzia uzito wa kutembea umbali mrefu.
Awali wananchi wa eneo hilo na vijiji jirani walilazimika kufuata huduma za afya Kata ya Katesh iliyopo umbali wa zaidi ya kilomita 20 kwenda na kurudi.
Akizungumza mbele ya kamati ya siasa ya wilaya ya Hanang iliyofika kituoni hapo kujionea utekelezaji wa agizo la serikali, Mganga mkuu wa Hospitali ya wilaya ya Hanag Dkt Boniface Manditi amesema huduma za afya zimeanza kupatikana tangu Jumatatu baada ya Waziri mkuu Kassim Majaliwa kutoa agizo siku ya Jumapili na kwamba kwa sasa wanasubiri vifaa vingine vya matibabu kutoka MSD.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Hanang Comrade Mathew Darema amemshukuru Waziri mkuu kwa kutembelea kituo hicho huku akiwaomba MSD kuharakisha kuleta vifaa tiba hivyo kama alivyoagiza Waziri mkuu ili vipatikane mapema katika kituoni hapo.
Naye mbunge wa Jimbo la Hanang Mhandisi Samweli Hhayuma amewataka watoa huduma katika Zahanati hiyo kutoa huduma nzuri kwa wananchi wake huku akiiomba halmashauri wilayani hapo kuongeza watoa huduma katika kituo hicho.
Baadhi ya wananchi waliofika kituoni hapo kupata huduma wameishukuru serikali na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali kwa kuwasogezea huduma za matibabu karibu kwa kuwa itawapunguzia gharama kubwa walizokuwa wanazitumia kwenye usafiri kufuata huduma.