**************************
Na. John Mapepele
Naibu Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Saidi Yakubu amesema maandalizi ya hafla ya utoaji wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati – Cornell ya Fasihi ya Afrika hapo kesho Januari 27, 2022 jijini Dar es Salaam ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi yamekamilika.
Akizungumza leo Januari 26, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akikagua ukumbi utakaotumika, Yakubu amekishukuru Chuo Kikuu cha Cornell cha nchini Marekani na kampuni ya Alaf kwa mchango wao wa kutambua na kukuza lugha la Kiswahili kupitia utoaji wa tuzo hizo.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mkakati wake wa kukikuza Kiswahili duniani.
“Kwa namna ya pekee tunampongeza Mhe. Rais wetu kwa mapenzi yake makubwa ya kukuza Kiswahili ambapo juzi tu akiwa kwenye sherehe na mabalozi amesema Sera ya nje zitazingatia kukuza Kiswahili .”Ameongeza Yakubu.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo anashughulikia Lugha, Dkt. Resani Mnata ametoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukuza lugha ya Kiswahili ili iweze kuenea katika nchi mbalimbali duniani.
Mtaalam anayeratibu tukio hilo la utoaji wa tuzo hizo Mustafa Hassanali amesema tukio hilo limeratibiwa kwa ujuzi wa hali ya juu ili kutoa hadhi inayositahili kwa tuzo hizo.