*************************
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Jan 26
Jeshi la polisi makao makuu limefanya uzinduzi wa matumizi ya mashine mpya za malipo kwa ajili kukusanya maduhuli ya serikali katika mkoa wa kipolisi Rufiji kwa kamanda wa polisi,mafisa,askari wa usalama barabarani pamoja na wahasibu.
Lengo la mashine hizo mpya zenye uwezo mkubwa Sambamba na mafunzo ni kuwajengea uwezo wa kutoa huduma kwa muda mfupi na kuondoa malalamiko yaliyokuwa yakijitokeza kipindi cha nyuma.
Hayo yalisemwa na Kamishna msaidizi wa jeshi la polisi Leonard Ngassa alipofanya ziara katika mkoa wa kipolisi Rufiji ,kutoa elimu kwa askari juu ya matumizi ya mashine mpya za kukusanya maduhuli ya serikali.
Alieleza, mashine hizi zitakuwa na uwezo mkubwa tofauti na awali kwani zimeongezewa baadhi ya mifumo ili kutoa huduma kwa haraka.
“Nia ya ziara yetu ni kutoa elimu na uzinduzi wa matumizi ya mashine hizi,Tunaishukuru Serikali kwa kuliwezesha Jeshi la polisi kwa ajili ya ununuzi wa mashine hizo, Tutaanza kutoa mafunzo nchi nzima kwa makamanda wa polisi,askari wa usalama barabarani, maafisa,wakaguzi na wahasibu” alifafanua Leonard Ngassa-Kamishna msaidizi wa polisi kutoka makao makuu.
Nae Kamishna msaidizi wa jeshi la polisi na Kamanda wa polisi mkoa wa kipolisi Rufiji ,Kungu Malulu alisema mashine hizo zitaongeza ufanisi wa kazi kwa askari pamoja huduma bora kwa wananchi wa mkoa wa kipolisi Ruiji.
“Tumepokea ugeni kutoka makao makuu kwa Ajili ya askari wetu ambapo pia tumepokea mashine hizi za kisasa”
Malulu alibainisha,kwa hakika ujaji wa mashine hizo utaboresha utoaji huduma na kuongezea ufanisi wa kazi kwa askari Rufiji na maeneo mengine.