Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba akiendesha kikao kazi ngazi ya Makatibu Wakuu na wakuu wa Taasisi kuhusu usimamizi na matumizi ya rasilimali maji katika mabonde ya Rufiji na Pangani ili kuwezesha upatikanaji wa Nishati endelevu, kilichofanyika tarehe 25 Januari, 2022 katika Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo Mtumba jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (kulia) akizungumza katika kikao kazi ngazi ya Makatibu Wakuu na wakuu wa Taasisi kuhusu usimamizi na matumizi ya rasilimali maji katika mabonde ya Rufiji na Pangani ili kuwezesha upatikanaji wa Nishati endelevu kilichofanyika tarehe 25 Januari, 2022 katika Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo Mtumba jijini Dodoma. Kushoto wa kwanza Naibu katibu Mkuu ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Abdallah Mitawi.
Dkt. Richard Muyungi (wa kwanza kushoto) kutoka Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) akiwasilisha mada mbalimbali wakati wa kikao kazi ngazi ya Makatibu Wakuu na wakuu wa Taasisi kuhusu usimamizi na matumizi ya rasilimali maji katika mabonde ya Rufiji na Pangani ili kuwezesha upatikanaji wa Nishati endelevu kilichofanyika tarehe 25 Januari, 2022 katika Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo Mtumba jijini Dodoma.
*******************
Hafsa Omar- Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amefungua rasmi kikao kazi ngazi ya Makatibu Wakuu na wakuu wa Taasisi wadau, kuhusu usimamizi na matumizi ya rasilimali maji katika mabonde ya Rufiji na Pangani ili kuwezesha upatikanaji wa Nishati endelevu.
Kikao hicho kimefanyika tarehe 25 Januari, 2022 katika Ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo Mtumba jijini Dodoma.
Makatibu Wakuu ambao wapo katika timu hiyo ni kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo na Umwagiliaji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maji, Wizara ya Ardhi, Nyumba Maendeleo ya Makazi, na Na wakuu taasisi zilizopo chini ya Wizara hizo.
Akizungumza katika kikao hicho Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Mramba alisema, Ikolojia ya Mabonde ya Rufiji na Pangani ni muhimu kwa ustawi wa Taifa kutokana na umuhimu wake katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta za nishati, maji, maliasili na utalii, mazingira, kilimo, mifugo, na uvuvi.
Aliongeza kuwa, Mabonde hayo ni muhimu kwa uzalishaji wa nishati ya umeme wa maji ambapo asilimia 36 ya umeme unaozalishwa nchini megawati 573 inatokana na chanzo cha maji katika Mabonde hayo.
Ambapo ameeleza, gharama za uzalishaji wa umeme kutokana na vyanzo vya maji ni wastani wa Shilingi 13 kwa uniti ikilinganishwa na gharama za uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia ambazo ni kati ya Shilingi 129 na 153 kwa uniti na kwa kutumia mafuta ya dizeli ni kati ya Shilingi 546 na 675 kwa uniti.
Aidha, alisema Ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa bei nafuu, Serikali imeendelea na jitihada za kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo vya maji vilivyopo nchini.
Katika jitihada hizo, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere megawati 2,115 ambapo baada ya kukamilika kwa mradi huu, uzalishaji wa umeme kwa vyanzo vya maji utakuwa ukichangia zaidi ya asilimia 73 ya umeme wote utakaokuwa ukizalishwa nchini.
Alifafanua kuwa, pamoja na umuhimu wa vyanzo vya maji katika uzalishaji wa nishati ya umeme, vyanzo hivyo vimekuwa vikikabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na uwepo wa shughuli za kibinadamu zisizoendelevu katika mabonde hayo pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alieleza kuwa, Kwa kutambua umuhimu wa kuhifadhi mabonde hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 13 Aprili, 2017, wakati huo akiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliagiza hatua za haraka zichukuliwe kwa lengo la kuokoa Ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu ili kuokoa mfumo wa Ikolojia wa Bonde la Mto huo.
Pia,alisema Wizara ya Nishati inatambua jitihada zilizochukuliwa na taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi kuhakikisha suala la utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji katika Mabonde ya Pangani na Rufiji unazingatiwa.
Vile vile, alisisitiza kuwa kwa kutambua jitihada zilizofanywa na Serikali na kwa kuzingatia maelekezo ya Viongozi wa Kitaifa kuhusu utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji nchini pamoja na uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme uliofanywa na Serikali hususani katika Mabonde ya Pangani na Rufiji.
Wizara ya Nishati iliandaa kikao kazi kwa ngazi ya wataalamu kuhusu uimarishaji wa usimamizi wa rasilimali maji katika Mabonde ya hayo, kikao hicho kilifanyika tarehe 16 hadi 21 mwaka jana, ambapo wataalamu hao walifanya kazi na kutoa mapendekezo mbalimbali ya usimamizi na matumizi ya rasilimali maji katika mabonde ya Rufiji na Pangani ili kuwezesha upatikanaji wa Nishati endelevu.