…………………………………………………..
Na Lucas Raphael,Tabora
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya magaharibi imekataza uvutaji wa aina yoyote ya bidhaa za tumbaku ambayo ni sigara, siga, sigarusi, misokoto, shisha, kiko na tumbaku ya unga, katika maeneo yote ya umma .
Kauli hiyo ilitolewa jana na Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya Magharibi ,Christopher Migoha wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya madhara bidhaa zitokanazo na mazao ya tumbaku.
Migoha alisema kwamba jukumu la udhibiti wa bidhaa za tumbaku ni la kisheria, ambapo Sheria ya Udhibiti wa Tumbaku, Sura 121 imekataza uvutaji wa aina yoyote ile ya maeneo ya Umma.
Aliyataja maeneo hayo ni yale yanayotoa huduma za afya, maktaba, mahali pa ibada, majengo au maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya mikutano ya kitamaduni na kijamii, shughuli za michezo na burudani.
Maeneo mengine aliyoyataja ni sehemu za huduma ya chakula, majengo ya ofisi, vyombo vya usafiri wa Anga, Ardhi , maji, mabanda ya maonesho, masoko, maduka makubwa na maeneo mengine yoyote yanayotumiwa na umma.
Migoha alifafanua kuwa Sheria kimeruhusu uvutaji wa bidhaa za tumbaku kwenye maeneo ya taasisi za elimu ya juu, majengo ya ofisi, hoteli, baa, migahawa na maeneo ya burudani ambayo yanatakiwa kuwa yametenga vyumba maalumu ya kuvutia bidhaa hizo.
Aidha Meneja huyo aliwataka wananchi wote wa mkoani Tabora kuzingatia utekelezaji wa Sheria hiyo ambayo imetakiwa kuanza mara moja maeneo yote ya Umma.
“Wamiliki wa maeneo hayo kuweka mabango ya makatazo na kwa yale maeneo yaliyoruhusiwa wahakikishe uvutaji wa bidhaa hizo unafanyika kwenye maeneo yaliyotengwa tu.”alisema Migoha
Hata hivyo aliwasihi kuendelea kushirikiana kikamilifu na TMDA katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za udhibiti wa matumizi ya bidhaa za tumbaku eneo ambalo linagusa maisha ya watanzania wengi wakiwepo watoto wetu chini ya umri wa miaka 18 ambao ni nguvu kazi ya taifa.