* Mawakala wanaowatafutia watanzania kazi zisizo na staha nje ya nchi waonywa*
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amekiagiza Kitengo cha Huduma za ajira (TaESA,) kuwafuata vijana katika taasisi za elimu na kuwaeleza fursa za ajira na namna ya kukabiliana na soko la ajira hasa wale wanaokaribia kuhitimu masomo yao kwa kuwapa mafunzo maalumu ya kuwajengeaa kujiamini, namna ya kuandaa wasifu wao pamoja na namna ya kukabiliana na waajiri wao.
Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea kitengo hicho kilichopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa kituo hicho kinafanya jitihada kubwa za kusajili wahitimu, kutoa mafunzo na kutafuta fursa za ajira katika kundi la vijana ambao wametakiwa kuwa waadilifu, wenye maadili, wazalendo na wenye kujituma pindi wanapopata fursa hizo.
”Nimeona hapa vijana wanajisajili na wengine kupata mafunzo hapa TaESA endeleeni kujitangaza nje ya Kanda zilizopo ili kila mtanzania apitiwe na fursa hii na sisi kama Wizara tutawaita kupitia majukwaa yetu mje kuwasilisha huduma mnazozitoa.” Amesema.
Prof. Ndalichako amesema fursa za uwekezaji ikiwemo ujenzi wa miundombinu ikiwemo madarasa na vituo vya afya zinazofunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan zinawalenga vijana kwa kiasi kikubwa na kwa kufanikisha hilo ni vyema kituo hicho kikaendelea kujitangaza zaidi.
Vilevile amesema, wana kazi ya kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025 kwa kuzalisha ajira ndani na nje ya nchi na kukitaka kituo hicho kuwafanyia uchunguzi wa kina mawakala wanaowatafutia watanzania kazi nje ya nchi kwa kuhakikisha kazi hizo zinakuwa na staha na utulivu.
”Wajiri na wekezaji wa miradi ya kimkakati pia watumie kituo hiki kwa kupata vijana ambao wameiva na wanaajirika na kwa mawakala wanaowatafutia watanzania kazi nje ya nchi zingatieni kanuni na sheria, Serikali ipo macho na haitamfumbia macho mwajiri atayewapa watanzania hasa vijana kazi zisizo na maadili.” Amesema.
Kuhusu mchakato wa kuwasajili vijana kwenda nchini Quatar kuhudumu katika fainali za kombe la dunia Waziri Ndalichako amesema zoezi linaendelea na watakaokwenda katika uwakilishi huo wakaipeperushe vyema bendera ya Tanzania kwa kuwa na nidhamu, kujituma, uadilifu na uzalendo kwa Taifa,
Awali akizungumza kuhusu kituo hicho Afisa Kazi Mkuu wa Kanda ya Mashariki na Pwani Jane Willium amesema, ujio wa mawaziri hao wanaosimamia sekta hiyo umewapa ari ya kufanya kazi zaidi katika kutekeleza sera ya ajira ya 2008 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020/2025 katika kutoa huduma za ajira na kunufaisha wananchi hasa vijana.
Bi. Jane amesema kuwa licha ya kutekeleza majukumu hayo wamekuwa na changamoto kadhaa ikiwemo wigo mdogo wa kutoa huduma hiyo ambayo inahitajika nchini kote lakini kumekuwa na kanda nne pekee hali inayopelekea kushindwa kufika katika maeneo mengine.
”Pia tumekuwa na changamoto ya ufinyu wa mafunzo ambayo yanatakiwa kufanyika mara kwa mara kutokana na ufinyu wa bajeti, pia tuna changamoto ya vitendea kazi hasa magari…tuna magari mawili pekee ambayo yapo hapa hii inatuwia vigumu kuwafikia wanaotafuta kazi na waajiri.” Amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira Joseph Sitta amesema, majukumu ya kituo hicho ni pamoja na kuwaunganisha wanaotafuta kazi na waajiri na mafunzo yaa utarajali kwa vijana pamoja na kuratibu watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi.
”Tuna kanda nne pekee nchini kote ambazo ni kanda hii ya Mashariki na Pwani inayoshughulikia mikoa ya Kusini, nyanda za juu Kusini, kanda ya Kaskazini, kanda ya ziwa na kanda ya magharibi….vijana watumie fursa zinazotolewa na kitengo hiki pamoja na Mawakala waliotangwazwa na Serikali katika kuwatafutia ajira nje ya nchi ili kuwa na uhakika na kuepuka sitofahamu zinazowakumba katika nchi za watu” Amesema.
Ameeleza kuwa hadi sasa wamefanikiwa kusajili wahitaji 52,771 katika kanzi data huku wahitaji 3209 wakipatiwa mafunzo, 425 wamepatiwa mafunzo ya utarajali na wahitaji 411 wamepatiwa fursa za kazi za kudumu na mkataba na kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kuandikisha vijana watakaokwenda kuhudumu nchini Quatar ambayo ina mkataba ba Serikali ambako fainalikombe la dunia zitafanyika.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako (katikati,) akizungumza mara baada ya kufanya ziara katika ofisi za Kitengo cha Huduma za ajira (TaESA,) na kukitaka kujitangaza zaidi ili vijana waweze kunufaika na huduma wanazotoa, kulia ni Naibu waziri wa Wizara hiyo Patrobas Katambi na kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira Joseph Sitta Nganga.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira Joseph Sitta Nganga akizungumza na wanahabari mara baada ya kuwapokea mawaziri wa Wizara wanaosimamia kitengo hicho na kueleza kuwa watashirikiana katika kuwafikia vijana wengi zaidi kupitia huduma zao.