Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne A Sagini akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwanzaburiga katika Jimbo lake la Butiama katika ziara yake Mkoani Mara, 24/01/2022. Amewahakikishia Watanzania kuwa Jeshi la Polisi ni Imara na lina watendaji wenye weledi wakufanya kazi zao.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne A Sagini amewataka Watanzania kutochukua sheria mkononi endapo wanamigogoro na familia zao au watu wao wa karibu bali kupeleka matatizo yao kwenye Vyombo vya Dola ili hatua za kisheria zifuate. Amesema hayo kwenye kikao na wananchi wanaoishi katika Jimbo lake la Butiama, kilichofanyika Kijiji cha Mwanzaburiga, Wilaya ya Butiama, Mara, 24/01/2022.
…………………………………………………..
Na Mwandishi wetu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne A Sagini ameelekeza Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutimiza wajibu wao baada ya kusikiliza changamoto za wananchi wa Kijiji cha Mwanzaburiga kilichopo Wilaya ya Butiama.
Akizungumza na wananchi waliolalamika kuhusu tukio la utapeli la kanisa la kijijini kwao, lililowashawishi kuchangia fedha kwa ajili ya ununuzi wa chakula kijijini Mwanzaburiga amewasihi kuwa waangalifu na kuelekeza Jeshi la Polisi kuchunguza usajili wa kanisa hilo.
“Uhalifu hauna dini wala kabila, kwahiyo yoyote anayefanya matendo ya kiuhalifu wa kuibia wananchi kwa mlango wa dini, vyombo viunavyohusika vihakiki Usajili wa Taasisi za Dini zilizolalamikiwa na hatua za kisheria zichukuliwe”
Naibu Sagini aliyasema hayo jana, wakati akizungumza kwenye mkutano na wananchi wanaoishi katika jimbo lake la Butiama, Kijiji cha Mwanzaburiga, Kata ya Kukirango, Mara.
Akitoa salamu za Rais Samia kwa wananchi wa Butiama, amewataka kupeleka migogoro yao kwenye vyombo vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe na kuepusha kuchukua Sheria mkononi.
“Jambo moja nataka kuwahakikishia watanzania tunalo Jeshi la Polisi imara, lenye watendaji walio na weledi wa kufanya kazi zao, mtu asifanye vitendo vya uhalifu akidhani atakuwa salama”.