Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akipanda mti kuashiria uzinduzi wa zoezi la mkoa huo kupanda miti 10,000 msimu huu wa mvua hafla iliyofanyika kijiji cha Sundu wilaya ya Kalambo jana.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selaman Jaffo akishiriki zoezi la upandaji miti pamoja na wananfunzi wa shule ya sekondari Kantalamba jana alopofanya ziara mkoa wa Rukwa.
Mkurugenzi wa shirika la Utunzaji Mazingira Rukwa (REMSO) Mzee Nkoswe Noel akizungumza jana kwenye hafla ya uzinduzi upandaji miti na ugawaji wa hati miliki za kimila kwa wananchi 400 wa Kalambo ikiwa ni kapmeni ya uhamasishaji jamii kutunza mazingira.
……………………………………………………………….
Na. OMM Rukwa
Mkoa wa Rukwa imezindua zoezi la upandaji miti kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuutunza mazingira na kurejesha uoto wa asili ambapo jumla ya miti Elfu Kumi imepandwa katika wilaya ya Kalambo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa alizindua kampeni hiyo jana (24.01.2022) katika kijiji cha Sundu wilaya ya Kalambo ambapo taasisi za umma na sekta binafsi zimeshiriki kupanda miti pembezoni na bwawa la maji la Sundu.
Mkirikiti amewataka viongozi wa taasisi zote za umma na binafsi kuendelea kupanda miti kwenye maeneo ya makazi na maeneo yaliyotengwa ili Rukwa iondokane na uharibifu wa mazingira na kurejesha uoto wa asili hatua itakayosaidia kuwa na uhakika wa mvua.
“Tujipange kupanda miti ili tuweze kupata faida kwa mazingira yetu kuwa bora na kuwa na uhahika wa hali ya hewa nzuri itakayoruhusu mvua nyingi kunyesha katika mkoa wetu kwani tumeharibu mno mazingira” alisema Mkirikiti.
Katika zoezi hilo lililoratibiwa na shirika lisilo la Kiserikali la Rukwa Environmental Organisation (REMSO)la Sumbawanga ambapo kupitia Mkurugenzi wake Mzee Nkoswe Zenol Noel liliratibu upatikanaji miti kutoka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Shamba la Miti Mbizi.
Kabla ya zoezi la upandaji miti Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aligawa Hati Miliki za Kimila za ardhi 400 kwa wananchi ambazo zimegharimu shilingi Milioni 65 kwa wananchi vijiji vya Ilambila(100), Kifone (100), Kamawe (100) na Kalaela (100) vilivyopo wilaya ya Kalambo.
Awali mapema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Seleman Jaffo alizungumza na wadau wa mazingira wa Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga ambapo aliwaeleza kuwa serikali ipo kwenye kampeni ya kuhamasisha upandaji miti kwa wanafunzi kwenye shule za sekondari na taasisi.
Dkt. Jaffo alibainisha kuwa amefurahishwa kuona mkoa wa Rukwa ulivyojipanga kuutunza mazingira ambapo wadau na serikali wameungana kuhakikisha wanafikia lengo la kupanda miti 10,000 mwaka huu.
“Tulizindua kampeni Maalum ya upandaji miti kwa kila mwanafunzi ambapo kwa mujibu wa takwimu Tanzania kuna wanafunzi milioni 14.1 wa shule za sekondari hivyo kila mmoja kupanda mti tutakuwa na miti Milioni 14.1 na kwa wanafunzi wa vyuo vya kati wapo takribani 400,000 hivyo kila mmoja atashiriki hatua itakayowezsha nchi kupanda miti Milioni 14.5 mwaka huu” alisisitiza Dkt. Jaffo.
Dkt. Jaffo akiwa mkoani Rukwa alishiriki kupanda miti pamoja na wanafunzi wa shule za sekondari ya Wasichana Sumbawanga na shule ya sekondari Kantalamba ambapo alisisitiza kila kaya kupanda miti mitatu kuzunguka mazingira yake.
Kuhusu kivutio cha utalii cha maporomoko ya maji Kalambo, Waziri Jaffo alitaka hatua madhubuti kuchukuliwa ili kuutunza mazingira ya eneo hilo yadumu vizazi na vizazi.
“Kalambo Falls haiwezi kuwepo endapo hatutatunza mazingira yake ikiwemo vyanzo vya maji. Endeleeni kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya taifa” alisisitiza Dkt. Jaffo.
Mwisho