Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geofrey Mizengo Pinda (kulia) akipata taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali alipotembelea banda la mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea Jijini Dodoma
******************
Na. Mwandishi Wetu-GCLA
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imepongezwa kwa kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa kubadilishana taarifa za uchunguzi (Laboratory Information Management System) unaojulikana kwa kifupi LIMS ambao utasaidia kuharakisha shughuli za kiutendaji kwa wadau wote wa haki jinai.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Geofrey Mizengo Pinda wakati alipotembelea banda la maonesho la mamlaka hiyo ili kujionea shughuli zake kwenye Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea Jijini Dodoma.
Naibu Waziri Pinda alibainisha kuwa GCLA ni sehemu ya Mahakama katika utendaji kazi kwa sababu baadhi ya kesi zinategemea ushahidi wa kimaabara kutoka kwenye mamlaka hiyo hivyo basi uwepo wa mfumo wa kielektroniki unarahisisha kazi za mahakama na kufanikisha utoaji haki kwa haraka.
“Nawapongeza sana Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuanzisha mfumo huo ambao Serikali tunaamini utarahisisha zaidi huduma za utoaji haki na uwepo wa mfumo kwenye ofisi za kanda za GCLA utawezesha kuzisogeza huduma zake karibu na zilipo huduma za mahakama hivyo kupunguza malalamiko ya ucheleweshaji haki kwa wananchi”, alisisitiza Mhe. Pinda.
Pia Mhe. Pinda amempongeza Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Ibrahim Juma na watendaji wote wa Mahakama kwa kuandaa maonesho hayo ambayo yanatoa nafasi kwa wananchi kupata elimu kuhusu haki zao na kuwasaidia kutatua kero zao kwa maslahi ya jamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Kwa upande mwingine Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Adam Mambi amepongeza juhudi za GCLA kwa kusimika vifaa vya Tehama katika ofisi zote sita za Kanda na kuunganishwa kwenye mfumo wa Mahakama ili kutoa ushahidi wa kitaalamu kwa njia ya mtandao hivyo kuondoa mlundikano wa kesi mahakamani ukilinganisha na hapo awali kabla ya mfumo huo.
“GCLA imefanikiwa kuunganishwa kwenye mfumo wa kielektroniki wa Mahakama ambao unawezesha kutoa ushahidi kwa njia ya mtandao bila ya mtaalamu wa maabara kusafiri kutoka hatua moja kwenda nyingine kwa ajili ya kutoa ushahidi mahakamani na hivyo kuokoa muda na gharama kwa Serikali,” alisisitiza Mhe. Mambi
Naye Kaimu Meneja wa Maabara ya Sayansi Jinai Sumu Bw. Kagera Ng’weshemi kutoka GCLA aliwaeleza wadau mbalimbali waliotembelea banda la GCLA kuwa licha ya mafanikio ya kuanzisha mifumo ya kielektroniki pia Serikali imeboresha huduma za mamlaka kwa kununua mitambo 9 ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli yenye thamani ya shilingi bilioni 6.6 ambayo imesaidia kupunguza muda wa kukamilisha uchunguzi wa kimaabara.
Aidha wananchi waliopata fursa ya kutembelea banda la GCLA wamepongeza maboresho ya utoaji huduma za mamlaka na kufurahia elimu waliyopata kutoka kwa wataalamu na kuahidi kufikisha elimu hiyo kwa jamii.