**************************************
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa agizo kwa wamiliki wa maduka binafsi ya dawa yaliyopo ndani ya mita 500 kutoka geti la kituo cha kutolea huduma za Afya kuyaondoa kabla ya tarehe 1 Julai 2022 kama kanuni ya mwaka 2020 ya uanzishaji wa maduka ya dawa inavyoelekeza.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo wakati alipotembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es salaam kuangalia namna huduma zinavyotolewa pamoja na kubaini changamoto mbalimbali wanazopitia wananchi katika kupata huduma Hospitalini hapo.
“Nalitaka Baraza la Famasi nchini kuanza kujiandaa kuchukua hatua, ikiwezekana kama duka la dawa lipo ndani ya mita 500 kutoka geti la kituo cha Afya, na maduka ambayo leseni yake inaisha kabla ya tarehe 30 Juni asiongezewe leseni yake mpaka atakapotoka ndani ya eneo la mita 500”. Amesema Waziri Ummy.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy amezitaka Hospitali za Rufaa za mikoa, Hospitali za Rufaa za kanda na vituo vingine vya Afya nchi nzima kuboresha huduma zao ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Ni lazima hospitali za rufaa za mikoa na hospitali za rufaa za kanda ziweke mikakati ya kuboresha huduma ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa sababu magonjwa mengine yangeweza kutibika kwenye mikoa na kanda, haiwezekani hata mgonjwa wa malaria aende Muhimbili”. Amesisitiza Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amewaahidi wananchi aliozungumza nao juu ya kuboresha huduma kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya nchini ili kuisaidia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kupokea rufaa ambazo zingeweza kuzuilika.
“Nataka niwaahidi Mhe. Rais Samia ameshaelekeza nguvu kwenye sekta ya afya, tunakwenda kuboresha huduma za Afya katika Hospitali za Halmashauri, Hospitali za Rufaa za Mikoa na Hospitali za Rufaa za kanda ili mtu akija Muhimbili aje na jambo ambalo limeshindikana kule chini.” Amesema Waziri Ummy.
Hata hivyo Waziri Ummy ameipongeza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kazi nzuri wanayofanya ikiwemo huduma za kibingwa na kibobezi licha ya kuwa na wagonjwa wengi.