Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akitoa maelekezo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 katika ya mgodi wa dhahabu wa Katavi uliopo wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo (wa tatu kushoto) akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali akitembelea na kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 katika ya mgodi wa dhahabu wa Katavi uliopo wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa mgodi wa Katavi wakati wa ziara yake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akisikiliza maelekezo kuhusu shughuli za uchimbaji katika mgodi wa dhahabu wa Katavi uliopo wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akikagua eneo linalotumika kwa shughuli za uchenjuaji wakati alipofanya ziara ya kukagua mgodi wa dhahabu wa Katavi uliopo wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
…………………………………………………………
Na Robert Hokororo, Katavi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amelekeza uongozi wa kampuni ya mgodi wa dhahabu wa Katavi kujenga bwawa la topesumu (TSF) la kuhifadhi tope sumu iliyotokana na hatua za uchenjuaji.
Dkt. Jafo ametoa maelekezo hayo jana alipotembelea mgodi huo uliopo Wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi na kutoa mwezi mmoja kwa uongozi wa mgodi huo kuanza utaratibu wa kupata Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) kwa ajili ya kujenga miundombinu hiyo.
Alisema kuwa Serikali inahitaji wawekezaji hususan katika sekta ya madini lakini hawana budi kufuata sheria za nchi zikiwemo za mazingira ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Aidha, waziri huyo alitoa angalizo kwa kubainisha kuwa mgodi huo upo katika eneo la hifadhi na pia karibu na mto hivyo endapo hatutajali mazingira tutajikitua madhara yanatokea kwa wanyama na binadamu.
“Kwanza kwa kutokuwa na cheti cha mazingira ni kosa sasa kwa vile tunawahitaji sana wawezekezaji ninatoa mwaka mmoja na miezi miwili tukijaaliwa TSF ianze kufanya kazi,” alisema.
Pia alipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Magharibi kwa kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara utendaji wa mgodi huo katika suala la kimazingira.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwamvua Mrindoko alimshukuru Waziri Jafo kwa kufanya ziara katika mgodi huo na kuahidi kuyasimamia kikamilifu maelekezo aliyotoa.
Alisema kuwa mkoa huo ni mingoni mwa mikoa mipya ambao unaendelea kujiimarisha kiuchumi hivyo wanaendelea kuwakaribisha wawekezaji ili mradi wanazingatia sheria ya mazingira.
Pia Meneja wa NEMC Kanda ya Magharibi, Bw. Benjamin Doto aliahidi kutilia mkazo maelekezo yote yaliyotolewa na waziri na kuwa kuahidi kutilia mkazo ili tarehe ya mwisho (deadline) ikifika yawe yametekelezwa.
Naye Kaimu Meneja Msaidizi wa mgodi huo, Bw. Twalib Mohamed Seif pamoja na kuishukuru Serikali aliahidi kutekeleza maelekezo yaliyotolewa ya kujenga bwawa la tope sumu na kusema wako tayari kufanya kazi kwa kufuata sheria za nchi bila kuathiri sekta ya mazingira.