Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza kwa njia ya mkutano mtandao (video conference) na wataalam kutoka Halmashauri mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu hao ya utekelezaji wa anwani za makazi uliofanyika jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dorosela Rugaiyamu akizungumza kwa njia ya mkutano mtandao (video conference) na wataalam wa Halmashauri mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar wakati Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi (aliyeketi kulia) akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu kwa ajili ya kutekeleza anwani za makazi uliofanyika jijini Dodoma.
Viongozi na wataalam waliopo kwenye vituo vinne vya mikoa ya Mwanza, Mbeya, Tanga na Zanzibar wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi (hayupo pichani) wakati akifunga mafunzo ya anwani za makazi na postikodi kwa wataalam hao kwa njia ya mkutano mtandao wakati akiwa ofisi za TTCL, jijini Dodoma.
…………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasilinano na Teknolojia ya Habari Dkt.Jim Yonazi,amefunga mafunzo ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi kwa waataalam zaidi ya 400 wa mikoa na halmashauri wa Tanzania bara na Zanzibar.
Dk. akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kufunga mafunzo hayo kwa njia ya mtandao amesema wataalam hao wanakwenda kuisaidia serikali kufikia azma ya kukamilisha utekelezaji wa mfumo kabla ya Mwezi Mei, 2022.
“Katika hili nitoe wito kwa viongozi na waratibu wa mradi huu katika ngazi ya wizara zinazotekeleza kuhakikisha wanakuwa bega kwa bega na wataalam hawa waliohitimu leo katika kutatua changamoto mbalimbali zitakazojitokeza wakati wote wa utekelezaji wa zoezi hili.
“Tulianza mafunzo haya mnamo tarehe 17 Januari, 2022 na leo tunakwenda kuhitimisha, ni takribani siku 7 ambazo mmejengewa uwezo juu ya Anwani za Makazi ni matumaini yangu kwamba mmeelewa vizuri mlichofundishwa na sasa mko tayari kuanza utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi kila mmoja katika eneo lake”amesema
Aidha, amesema kuwa ni matumaini ya viongozi pamoja na serikali kwa ujumla kuwa sasa wamepatikana wataalam mahiri wenye ufanisi wa hali ya juu kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi.
“Nafahamu kwamba wengi wenu mnatoka katika Halmashauri ambazo pengine nyie ndio watendaji mnaotegemewa zaidi katika ofisi zenu, jambo la anwani za makazi ni jambo la Kitaifa lenye maelekezo na lina ukomo wa utekelezaji.
“Kwa msingi huo nitumie fursa hii kuwaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, kuwaondolea majukumu mengine wataalam waliopatiwa mafunzo katika kipindi hiki ambacho tunaendelea na utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi ambao kimsingi wataalam hao ndio waratibu wa utekelezaji katika maeneo yao”amefafanua Yonazi
Hata hivyo,amewataka kuyatumie vyema maudhui ya mafunzo waliyoyapata katika kufanikisha utekelezaji wa mfumo huo kwenye maeneo yao ndani ya muda uliopangwa.