MBUNGE wa Jimbo la Gando Salim Mussa Omar,akielezea namna alivyotekeleza Ilani ya CCM ya Mwaka 2020/2022 katika jimbo hilo.
MJUMBE wa Sekretariet ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Ndg.Gilbert Kalima, akizungumza na Wana CCM wa Tawi la Gando mara maaba ya kufungua Tawi hilo katika ziara ya Kikazi ya kuimarisha Chama ya Wajumbe wa Sekretariet hiyo katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.(Picha na Is-haka Omar- Afisi Kuu CCM Zanzibar).
*************************
NA IS-HAKA OMAR,PEMBA.
MJUMBE wa Sekretariet ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndg.Gilbert Kalima, amesema falsafa ya Uchumi wa Blue ikitekelezwa kwa vitendo itawainua kiuchumi wananchi wengi visiwani Zanzibar.
Kauli hiyo ameisema mara baada ya kufungua Tawi la Gando lililopo katika Jimbo la Gando Wilaya ya Wete, amesema falsafa hiyo imejaa vitu vya msingi ambavyo vikitekelezwa kwa haraka vitawatoa wananchi katika wimbi la umasikini.
Kalima, alieleza kwamba mambo hayo hasa miradi ya viwanda vidogo vidogo,viwanda vikubwa na fursa ya matumizi ya teknolojia katika sekta za uvuvi,kilimo na uwekezaji ndio uti wa mgongo wa kukuza kwa haraka uchumi wa Nchi.
Aliwambia wananchi wa Jimbo la Gando kwamba watumie vizuri fursa ya uchumi wa blue ili waweze kunufaika na kipato kikubwa kitakachotokana na matumizi mazuri ya uvuvi na kilimo cha kisasa.
Kalima ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, alieleza kwamba Sera hiyo ya uchumi wa blue iliyoasisiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, imebeba fursa mbalimbali za kuwakomboa wananchi kiuchumi.
Katika maelezo yake Katibu Kalima, aliwataka Wana CCM wa Jimbo hilo na maeneo jirani wawe wa kwanza kunufaika na fursa hiyo kwa kuanzisha vikundi vingi vitakavyochangamkia fursa zinazotokana na uchumi wa blue.
“ Wanachama wenzangu Mheshimiwa Rais Mwinyi, amekuja na falsafa hii ya uchumi wa blue na tunaona namna anavyopambana kuhakikisha wananchi wanapata zana za kisasa katika masuala ya uvuvi na kilimo sambamba na kufungua fursa za uwekezaji wa wageni na wazawa.
Wito wangu kwenu muhakikishe mnamuunga mkono na kuwakataa baadhi ya watu wenye nia na dhamira ya kumkwamisha, kwani manufaa yanayopatikana ni kwa maslahi ya nchi na sio maslahi binafsi.”, alieleza Katibu Mkuu huyo wa Wazazi Kalima.
Pamoja na hayo aliwambia wananchama hao kwamba wanatakiwa kuendelea kuhamasisha wananchi wajiunge na Chama ili kuongeza idadi ya Chama hicho.
Aliwapongeza Mbunge,wawakilishi na Wanachama wa CCM kwa kazi kubwa ya kujenga Tawi la Kisasa ambalo litatumika kwa ajili ya Vikao vya Chama na shughuli nyingine muhimu za kiutendaji na kiuongozi.
Pamoja na hayo aliwataka Wana CCM kuendelea kujadili kwa kina namna ya kulinda Amani na Utulivu uliopo nchini ili usichezewe na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo.
Amewataka Viongozi waliopewa dhamana ya uongozi bila kujali tofauti za Kisiasa wachape kazi kwani ndio kipimo sahihi cha kuwavuta wapinzani kujiunga na Chama Cha Mapinduzi, kwani kitakuwa kinatoa majibu sahihi ya maswali na mahitaji yao.
Kalima, alitamka wazi kwamba CCM ni Chama Kiongozi na chenye nguvu kisiasa na kisera hivyo kinajikita katika kujadili,kutekeleza na kupanga mambo ya maendeleo ya watu wala hakina muda wa kujadili fitna na majungu.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kukutana na kuzungumza na Wanachama kwa ngazi za mashina ambao ndio chimbuko la wanachama hai wa CCM kusikiliza changamoto,maoni na mafanikio yao ili Chama kiweze kujipanga zaidi katika mikakati yake.
Alieleza kwamba malengo mengine ni kuakagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 ambayo ndio uti wa mgongo wa maendeleo ya Nchi.
Sambamba na hayo aliwataka Wana CCM kuendelea kuchapa kazi bila kuchoka ili kuenzi kwa vitendo malengo ya Waasisi wa Mapinduzi ya Mwaka 1964, walioikomboa Zanzibar kutoka katika mikono ya Watawala wa kigeni na kujitawala wenyewe.
Aliwakumbusha umuhimu wa kuhakikisha wanahamasisha Wananchi kushiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makaazi ya mwaka huu 2022 ili serikali ipate nafasi ya kupamba vizuri mahitaji ya wananchi kwa mujibu wa idadi yao.
Aliwapongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kwa kasi yake ya kiutendaji kwa kujengwa zaidi ya madarasa 200 ya shule ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake za kuendeleza kwa kasi miradi ya Kimkakati ambayo italeta tija na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Gando Salim Mussa Omar, amesema anaendelea kutekeleza vyema Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, kwa kuwanunulia wavuvi nyavu zenye kiasi cha shilingi milioni 18 ili wanufaike na dhana ya uchumi wa blue.
Aidha Mbunge huyo alisema ametoa kiasi cha shilingi milioni 45 kwa ajili ya ujenzi wa skuli katika shule ya mkote,kusimamia ujenzi wa barabara tatu za ndani za kiwango cha lami.
Amesema anaendelea kutafuta ufumbuzi wa tatizo la maji safi na salama katika maeneo mbali mbali ambapo ametoa vifaa vya kusambazia maji vyenye thamani ya milioni 70.
Kwa upande wa Mwakilishi wa Jimbo hilo Mariam Thani, amesema kwa upande wake ameshiriki katika kuchangia fedha za ujenzi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Jimbo hilo.