Home Mchanganyiko WATU 5 FAMILIA MOJA WAUAWA KIKATILI NA WATU WASIOJULIKANA BAHI DODOMA

WATU 5 FAMILIA MOJA WAUAWA KIKATILI NA WATU WASIOJULIKANA BAHI DODOMA

0

………………………………………………

Na.Alex Sonna,BAHI

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Onesmo Lyanga,amethibitisha kuwa watu watano wa familia moja wakazi wa Kijiji cha Zanka Wilayani Bahi Mkoani Dodoma wameuwawa kikatili na watu wasiojulikana huku miili yao ikikutwa ndani nyumba yao ikiwa imeanza kuharibika.

Akizungumza na waandishi wa habari Usiku katika eneo la tukio amedai kuwa taarifa za awali zinaonyesha watu hao wameuwawa na watu wasiojulikana.

Walio kufa katika tukio hilo ni Hoseah Kapande ambaye ni baba wa familia hiyo na mkewe Paulina Kapande.

Wengine ni watoto wawili na mjukuu mmoja ambao ni Isack Kapande mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Agnes Kapande mwanafunzi wa darasa la tatu pamoja na mjukuu aliyejukana kwa jina la Heltony ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne.

Kamanda Lyanga,amesema kuwa  kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa mauaji hayo huku likiwataka wananchi wa eneo hilo kuwa watulivu katika kipindi hichi.

Aidha, Kamanda Lyanga amewata wananchi wa eneo hilo kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanatoa taarifa za matukio mbalimbali ya kihalifu yanayofanywa ndani ya jamii.

“Kumekuwa na matukio mengi ya mauaji ya kificho, Jeshi limejipanga kuwasaka wahalifu wa matukio hayo,”amesema Kamanda Lyanga.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka, ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa matukio hayo ambayo yanakatisha  maisha ya watu.

Aidha amewataka  ndugu kutoa ushitikiano wa kuwasaka wahalifu waliofanya tukio hilo ambalo si la kiungwana lililosababisha familia hiyo kupoteza maisha.

Mtaka amesema kuwa wanahitaji kuona Dodoma inakuwa salama na kuongeza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kupambana na wahalifu hao ambao wanaikatili jamii.

Naye mdogo wa marehemu Ernest Kapande amesema kuwa mara ya mwisho kumuona marehemu na familia yake ilikuwa Januari 20 mwaka huu.

Amesema baada ya kumuona siku hiyo hawajaonan tena hadi juzi ambapo alipata taarifa kuwa kaka yake pamoja na familia yake nzima wamekutwa wameuwawa ndani ya nyumba yao.

“Mimi marehemu ni kaka yangu mara ya mwisho kumuona ilikuwa ni juzi lakini baada ya hapo hatukuonana tena”amesema

 Amesema taarifa za kifo cha kaka yake amezipata kutoka kwa mtoto wake ambaye alimpigia simu kuwa baba yake mkubwa amekutwa amekufa ndani ya nyumba na familia yake.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho alisema taarifa za tukio hilo wamezipata juzi majira ya saa 10 jioni mara baada ya watoto washule kutoa taarifa.

“Watoto wadogo washule ndiyo walianza kupiga kelele baada ya kuona miili ya marehemu wakiwa ndani na wameanza kutoa harufu ndipo taarifa na sisi tukazitoa kwa mkuu wa kituo cha polisi”alisema mwenyekiti huyo

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo Neema Mbuva amesema mauaji hayo yemechangia kwa kiasi kikubwa kukatisha ndoto za wanafamilia hao bila sababu ya msaingi.

Amesema wao kama wanakijiji wa eneo hilo wamesikitishwa na mauaji hayo na kulitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi ili kuwabaini wahalifu hao.

Hli ni tukio la tatu la mauaji mkoani Dodoma ukiacha yale ya awali ambapo wanawake wawili waliuwawa na wazazi wenzao kutokana na ugomvi wa kifamilia.