Na Mwandishi Wetu
PROSPER Remmy Magali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA) na Mkurugenzi wa Ubunifu na Uendelezaji Miradi katika kampuni ya ENSOL TANZANIA LLIMITED, amewapa wajasiriamali zawadi ya kuanzia mwaka kwa kuzindua kitabu kiitwacho: ‘ANZA, KUA NA STAWI KATIKA MIRADI NA BIASHARA: Mbinu za Kipekee za Kuanzisha, Kukuza na Kuendeleza Miradi na Biashara.’
Uzinduzi huo umeafanyika katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam ukiwashirikisha wajasiriamali, taasisi na wasomi wa kada mbalimbali na shuhuda za safari ya ujasirimali kuelekea mafanikio zikatolewa.
Huku kikitoa mfano wa Mfanyabiashara maarufu Tanzania na barani Afrika; Salim Said Bhakresa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Dk Regnald Mengi, kitabu hicho kilichofadhiliwa na kampuni ya ENSOL na dibaji yake kuandikwa na Profesa Geoffrey R. John wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kinaelezea kwa kina Mbinu za Kisasa za Kuanzisha Miradi na Misingi ya Mafanikio Katika Biashara na Maisha.
Mengine yanaoelezwa katika kitabu hicho ni Azimio la Arusha na Fursa za Ujasiriamali; Umuhimu na Mbinu za Kupata na Kutumia Mikopo kwa Manufaa Ili Kupata Maendeleo; Visingizio Vinavyowafanya Watu Washindwe Kuanzisha Biashara au Miradi; Mbinu za Kugeuza Matatizo/ Changamoto Kuwa Fursa na Mbinu za Kupunguza Kiwango cha Kodi Bila Kuvunja Sheria za Nchi.
Katika uzinduzi wa kitabu hicho ambacho sasa kipo sokoni kwa Sh 10,000, Mwandishi Prosper Magali anayepatikana kwa simu: 0762508917, alisema: “Watu wengi wanafikiria, wanatamani, wanapenda na wanataka kufanya ujasiriamali, lakini wanakosea katika kuanza… Anza na kile ulicho nacho hata kama ni kidogo na kisha kiwekee mikakati ili kikue na kuongezeka.”
Akaongeza: “Yaliyo katika kitabu hiki yakisomwa na kuzingatiwa, yatatoa hamasa kwa watu wengi zaidi na kutoa msukumumo mpya wa kufungua biashara, kuzimiliki na kuzifanya kuwa bora na zenye mafanikio.”
Mkurugenzi wa Taasisi ya Uongpozi na Maendeleo ya Ujasiriamali, Dk Donath Olomi aliyekuwa mgeni rasmi, alipongeza ubora wa kitabu hicho akisema kimendikwa na mtu sahihi aliyesoma, akajifunza na sasa ana uzoefu kwa kuwa naye ni mjasiriamali.
Alisema siri ya kukuza biashara ni kupata mtaji zaidi kupitia mikopo na uwekezaji kwani hakuna biashara au miradi iliyofanikiwa bila mkopo.