Meneja wa wakala wa barabara za vijijini na mijini(Tarura)wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Oscar Mussa kulia,akitoa taarifa ya ujenzi wa miradi ya barabara katika wilaya hiyo kwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Mbinga,wa pili kushoto Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Mbinga Beda Hyera.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wa pili kulia,akikagua ujenzi wa Barabara ya lami ya Mbuyula-Ikulu ndogo yenye urefu wa km 1 inayojengwa na wakala wa Barabara za vijijini na mijini(Tarura) wilaya ya Mbinga wakati wa ziara yake kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo,kushoto kwake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo,wa kwanza kushoto Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge katikati akimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo wa kwanza kulia wakati Mkuu wa mkoa alipotembelea ujenzi wa mradi wa barabara ya lami ya Mbuyula Ikulu ndogo inayojengwa na wakala wa barabara za vijijini na mijini Tarura wilayani Mbinga.
………………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Mbinga
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,amekagua mradi wa ujenzi wa Barabara ya lami ya Mbuyula hadi Ikulu ndogo katika Halmashauri ya Mji Mbinga inayojengwa na Wakala wa Barabara za vijijini na mijini Tarura wilaya ya Mbinga na kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo.
Mkuu wa mkoa ameipongeza Tarura kwa matumizi mazuri ya fedha na kwa kutumia wakandarasi wa ndani katika utekelezaji wa barabara zinazojengwa katika wilaya ya Mbinga.
Alisema, jitihada hizo za kuwatumia wakandarasi wazalendo ni uamuzi mzuri na sehemu ya mpango wa Serikali ya awamu ya sita kuwajengea uwezo wakandarasi wetu ili waweze kufanya kazi kwa weledi na viwango vya hali ya juu na kuwaimarisha katika utendaji wa kazi zao.
Hata hivyo, amewataka wakandarasi kuhakikisha wanajenga barabara na miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo kwa ubora ili Serikali iendelee kuwaamini kwa kuwapa na kuwatumia katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Alisema, ni muhimu kwa Wataalam wa ndani kutanguliza uzalendo wanapotekeleza miradi inayotokana na fedha zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ili miradi hiyo ilete tija na kuharakisha uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya,mkoa na Taifa.
Meneja wa Tarura wilaya ya Mbinga Oscar Mussa alisema,kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga Sh.1,941,120,000.00 kwa ajili ya matengenezo ya barabara kati ya hizo Sh.941,120,000.00 zimetengwa kwa miradi ya ukarabati wa barabara,makaravati,madaraja,usimamizi na utawala na Sh.1,000,000.00 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Mji Mbinga.
Kwa upande wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Mussa alisema, katika bajeti ya Mwaka 2021/2022 Tarura imetengewa Sh.2,336,760,306.21 kwa ajili ya matengenezo ya barabara,kati ya hizo Sh.781,550,306.21 zitatumika kukarabati barabara,makaravati na madaraja na Sh.1,500,000.00 za miradi ya maendeleo.
Akizungumzia ujenzi wa barabara ya Mbuyula- Ikulu ndogo inayojengwa kwa kiwango cha lami Mussa alisema, Tarura ilipokea Sh. 500,000,000.00 ambapo kazi ya ujenzi ilianza Mwezi Septemba 2021 na utekelezaji wake umefikia asilimia 95.
Kwa mujibu wake, Mkandarasi wa barabara hiyo ni mzawa kampuni ya Ovans Construction Ltd na kwa sasa kazi zinazoendelea katika ujenzi wa mradi huo ni umaliziaji wa mitaro.
Mussa alitaja barabara nyingine inayojengwa kwa kiwango cha lami ni Longa-Kipololo hadi Litoha yenye urefu wa km 1 kwa gharama ya Sh.500,000,000.00 ambayo inatarajia kukamilika Mwezi huu.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kuendelea kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi yam waka 2020-2025 kwa kuipa fedha Tarura ambazo zimewezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa barabara katika wilaya ya Mbinga.