********************
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde (Mb) leo tarehe 21 Januari, 2022 akiwa na Balozi wa India nchini Tanzania, Mheshimiwa Binaya Srikanta Pradhan
wameshuhudia usafirishaji wa parachichi kuelekea nchini India kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikiwa ni mzigo wa pili unaokamilisha tani 2.2 tangu parachichi ianze kusafirishwa Januari,2022.
Mhe. Mavunde ameeleza kwamba tukio hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi wakuu wa Nchi akiwemo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020-2025 ambayo imeielekeza serikali kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde ameeleza kuwa Tanzania kwa sasa inazalisha wastani wa tani 40,000 za parachichi ambapo ni tani 9,500 pekee ambazo zinauzwa nje ya nchi.
“Nchi yetu ina fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa parachichi,tutaendelea kuhamasisha wakulima wetu kuzalisha kwa tija na kufuata kanuni za kilimo bora” aliongeza Mhe. Mavunde.
Vilevile, Mhe. Mavunde aliongeza kuwa, kupitia bajeti ya mwaka ujao wa fedha, Wizara imedhamiria kuanzisha Kituo Maalum (Common user facility) kati ya Mkoa wa Iringa na Njombe. Alieleza kuwa, Kituo hicho kitafanya kazi ya kukusanya parachichi, kuchambua (sorting) kwa kupanga madaraja na kuhifadhi kwenye vifungashio vyenye lebo ambayo itakuwa inaonesha uasili wa bidhaa hiyo.
“Kwa kufanya hivyo tutasaidia kuongeza wigo wa masoko ya parachichi zetu, tofauti na sasa ambapo parachichi yetu asilimia kubwa inatoroshwa na kuuzwa nje kama bidhaa isitoka Tanzania” alisema.
“Mkakati mwingine tuliodhamiria kama Wizara ni kuanzisha Mnyororo wa Kijani (Green channel) kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa mazao ya horticulture kuanzia shambani mpaka yanapofika kwenye kituo cha kusafirishia kwenda nje ya nchi”, aliongeza Mhe. Mavunde.
Naibu Waziri Mavunde alisema kuwa, tayari Wizara ya Kilimo imeanza kufanya mazungumzo na Wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Sekta binafsi kwa lengo la kuhakiksha mfumo huo endelevu wa mnyororo wa kijani au Green Channel unaanzishwa nchini.