Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida
JESHI la Polisi mkoani hapa linawashikilia watuhumiwa 16 kwa mahojiano kufuatia tukio la kufukuliwa na kuibwa kwa mwili wa mtoto Christian Samson mwenye umri wa mwaka mmoja na mwezi mmoja aliyekuwa amezikwa kwenye makaburi ya Kipondoda yaliyopo kitongoji cha Kipindoda, Tarafa na Wilaya ya Manyoni.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida Kamisha Msaidi (ACP) Stella Mutabihirwa kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema baada ya kupata taarifa hizo jeshi hilo kupitia makachero wake lilifika katika eneo la tukio na kufanya uchunguzi wa awali na kujiridhisha kuwa ni kweli kaburi lilifukuliwa na mwili huo kuibwa huku jeneza likiachwa tupu.
Mutabihirwa alieleza kuwa mnamo Januari 18 mwaka huu majira ya saa 1:15 asubuhi Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida lilipokea taarifa kuwa usiku wa kuamkia tarehe na mwezi huo kwenye eneo la makaburi hayo mwili wa marehemu, ambaye ni mgogo, mkristo na mkazi wa Kipondoda aliyefariki Januari 15 mwaka huu kwa maradhi-na kuzikwa siku iliyofuata-ulifukuliwa na kuchukuliwa kutoka kwenye jeneza kutoka kwa watu wasiofahamika.
Alisema watuhumiwa wa tukio hilo baada ya kufanya uhalifu huo walitokomea kusikojulikana hadi pale Jeshi la Polisi lilipopata taarifa hizo na kutuma timu ya makachero wake ambao kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji na raia wema lilifanya msako mkali ambapo siku sita baada ya maziko-yaani Januari 21 majira ya saa 6:15 usiku mwili wa marehemu ulipatikana ukielea kwenye kisima cha maji chenye urefu wa futi 12 kilichopo jirani na eneo la kata hiyo.
’’Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa 16 kwa mahojiano. Mwili wa Marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu katika hospitali ya Wilaya ya Manyoni na kukabidhiwa kwa ndugu kwa hatua za mazishi,’’ alisema Mutabihirwa.
Hata hivyo kufuatia tukio hilo Kamanda huyo aliwasihi wananchi kuachana na kujihusisha na masuala ya imani za kishirikina na kutenda matendo mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu kutokana na tukio tukio kujionyesha dhahiri kuwa na viashiria vya moja kwa moja vya imani hizo.