Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala (wa pili kulia) akipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine Major Songoro kulia wakati alipotembelea yadi ya Songoro Ilemela mjini Mwanza kukagua ukarabati unaoendelea wa vivuko vya MV. MUSOMA, MV. TEMESA pamoja na MV. SABASABA. Vivuko hivyo vinafanyiwa ukarabati mkubwa na vinatarajiwa kurejea kutoa huduma hivi karibuni. Wa tatu kushoto ni meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Hassan Karonda.
Mkurugenzi wa kampuni ya Songoro Marine Major Songoro kushoto akimuonyesha kitu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala (katikati) wakati alipotembelea yadi ya Songoro Ilemela mjini Mwanza kukagua maendeleo ya ukarabati wa vivuko vya MV. MUSOMA, MV. TEMESA pamoja na MV. SABASABA ambavyo vinafanyiwa ukarabati mkubwa na kampuni hiyo, vivuko hivyo vinatarajiwa kukamilika hivi karibuni. Kulia ni meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Hassan Karonda.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala (katikati) akitoa maagizo kwa meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Hassan Karonda kulia wakati akikagua ukarabati unaoendelea wa vivuko vya MV. MUSOMA, MV. TEMESA pamoja na MV. SABASABA vinavyofanyiwa ukarabati mkubwa na kampuni ya Songoro katika yadi yake iliyopo Ilemela Mkoani Mwanza. Kushoto ni Mkurugenzi wa kampuni ya Songoro Marine Major Songoro.
Mkurugenzi wa kampuni ya Songoro Marine Major Songoro aliyenyoosha mkono akimpa maelezo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala (wa pili kulia) wakati akikagua kivuko cha MV.SABASABA ambacho kinafanyiwa ukarabati mkubwa na kampuni ya Songoro katika yadi yake iliyopo Ilemela Mkoani Mwanza. Mtendaji Mkuu pia alikagua vivuko vya MV.TEMESA na MV. MUSOMA ambavyo pia vinafanyiwa ukarabati mkubwa. Kulia ni meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Hassan Karonda.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala (katikati) akitoa maagizo kwa meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Hassan Karonda kulia wakati akikagua ukarabati unaoendelea wa kivuko cha MV. SABASABA kinavyofanyiwa ukarabati mkubwa na kampuni ya Songoro katika yadi yake iliyopo Ilemela Mkoani Mwanza. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa kampuni ya Songoro Marine Major Songoro.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala kulia, meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Hassan Karonda katikati na Mkuu wa kivuko cha Kigongo Busisi Mhandisi Aticki Abdallah wakishuka kutoka kwenye kivuko cha MV. MISUNGWI mara baada ya kumaliza kukikagua, kivuko hicho kinatarajiwa kuondolewa majini kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa hivi karibuni ambapo kitapelekwa katika yadi ya Songoro iliyopo Ilemela Mkoani Mwanza.
Meneja wa TEMESA Mwanza Mhandisi Hassan Karonda kushoto akimueleza jambo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala kulia wakati walipokuwa wakikagua utendaji kazi wa kivuko cha MV. TEGEMEO kinachotoa huduma katika Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa kati ya Kaunda, kisiwa cha Maisome na Nkome Mkoani Mwanza.
Abiria wakishuka kutoka katika kivuko cha MV. UJENZI kinachotoa huduma kati ya Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza. Kivuko hicho ambacho kinatarajiwa kuondolewa kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa kina uwezo wa kubeba abiria 330 na magari 10 sawa na tani 85.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO
……………………………………………………………….
Na. Alfred S. Mgweno (TEMESA)
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro Kilahala amewataka watumishi wa Wakala huo kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi ili kuongeza uzalishaji na kuongeza pato la Wakala huo.
Mtendaji Mkuu ametoa maaagizo hayo wakati wa ziara yake kiutendaji aliyoifanya mwanzoni mwa wiki hii katika Mikoa ya Mwanza, Geita na Mara ambapo ametembelea karakana za mikoa hiyo pamoja na vivuko ambavyo vinatoa huduma katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo.
Akizungumza na watumishi wa vituo na mikoa hiyo kwa nyakati tofauti, Mtendaji mkuu aliwataka watumishi hao kujiuliza ni namna gani wanaweza kufanya ili kuboresha uzalishaji na kukuza kipato cha vituo vyao.
‘’Tuongeze ufanisi katika maeneo yetu ya kazi ili kuhakikisha tunakua bora zaidi katika utendaji kazi wetu,’’ alisema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa changamoto walizotoa watumishi wa mikoa hiyo zipo na zitaendelea kuwepo hivyo ni jukumu lao pamoja na watumishi wenzao kuhakikisha wanazishinda changamoto hizo na kuboresha uzalishaji wao.
Aidha akiwa katika ziara hiyo Mtendaji Mkuu pia aliwaagiza mameneja hao kuhakikisha wanafanya maboresho ya namna wanavyokusanya mapato ya vituo vyao na kuondoa dhana ya utegemezi kutoka makao makuu kwani dhana hiyo inawazorotesha kufikia malengo wanayopaswa kuyafikia.
‘’Tujitahidi kuondoa fikra kwamba kuna ruzuku na tujipambanue katika kuhakikisha tunaongeza mapato kwa ajili ya kujiendesha wenyewe, pambaneni kwa taswira hiyo, tujiulize tufanye nini ili kuongeza mapato yetu’’, alisema Mtendaji Mkuu na kuwataka watumishi hao watafakari watakapoondoka TEMESA, watakumbukwa kwa lipi na vizazi vijavyo.
Mtendaji Mkuu alianza ziara hiyo ya kiutendaji kwa kutembelea karakana ya TEMESA Mkoa wa Mwanza, Yadi ya Songoro ambapo alikagua ukarabati wa vivuko vya Wakala huo unaofanywa na kampuni ya Songoro ambapo vivuko vya MV.SABASABA, MV.TEMESA pamoja na MV. MUSOMA vinafanyiwa ukarabati mkubwa baada ya kufikia muda wake wa ukarabati.
Mtendaji Mkuu pia alitembelea kivuko cha MV. KOME II kinachotoa huduma kati ya Nyakaliro na Kome, aidha alitembelea pia Wilayani Buchosa ambapo amekagua kivuko cha MV.TEGEMEO kinachotoa huduma kati ya Kaunda, kisiwa cha Maisome na Nkome. Kivuko cha MV. TEGEMEO kilifanyiwa ukarabati mkubwa hivi karibuni na kinaendelea vizuri kutoa huduma katika eneo hilo.
Aidha Mtendaji Mkuu pia alitembelea kivuko cha Kigongo Busisi na kukagua vivuko vyote vinavyotoa huduma katika kituo hicho ikiwemo kivuko cha MV. MISUNGWI ambacho kinatarajiwa kuondolewa kwenye maji hivi karibuni kwa ajili ya kupelekwa katika yadi ya Songoro kufanyiwa ukarabati mkubwa, alitembelea kivuko cha MV. CHATO II ambapo pia alikagua ujenzi wa jengo la abiria kupumzikia (Waiting Lounge) linalojengwa katika kituo hicho, alipata pia wasaa wa kukagua maegesho ya kivuko cha MV. TEMESA yaliyopo Luchelele, alitembelea kivuko cha MV. UKARA II kinachotoa huduma kati ya Bugorola na Ukara,
Vilevile alitembelea Mkoani Mara ambapo alikagua karakana ya Mkoa huo, alitembelea kivuko cha MV. UJENZI kinachotoa huduma kati ya Rugezi Wilayani Ukerewe na Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara, pia alikagua kivuko cha MV. CHATO I ambacho kinatoa huduma kati ya Kinesi na Musoma mjini kikiwa ni mbadala wa kivuko cha MV. MUSOMA ambacho kinafanyiwa ukarabati mkubwa katika yadi ya Songoro.
Mtendaji Mkuu alimalizia ziara yake katika kivuko cha MV. ILEMELA kinachotoa huduma kati ya Kayenze, visiwa vya Bezi na Ukerewe ambapo pia alikagua jengo la abiria kivukoni hapo na kuzungumza na watumishi wa kivuko hicho.