Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza katika kikao cha wataalam wa Sekta ya Mifugo kilichojadili hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ambapo amawataka wataalam hao kukusanya fedha ili kufikia malengo yaliyowekwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 ya kukusanya bilioni 50. Kikao hicho kimefanyika Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda akizungumza wakati wa kikao cha wataalam wa sekta ya mifugo kilichojadili kuhusu hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali. Bw. Nzunda amewataka wataalam hao kuwasilisha taarifa za makusanyo ya maduhuli kila mwezi. Kikao hicho kimefanyika Jijini Dodoma.
Mhasibu Mkuu wa Sekta ya Mifugo, Bi. Veronica Kishala akiwasilisha mada kuhusu hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwenye sekta ya mifugo kwenye kikao cha Waziri wa Mifugo na Uvuvi na wataalam wa sekta hiyo kilichofanyika Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga akitoa ufafanuzi wakati wa kikao cha Waziri na Wataalam wa Mifugo wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kilichofanyika Jijini Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) na Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo, Bw. Tixon Nzunda (kushoto) wakifuatilia mjadala uliokuwa ukiendelea wakati wa kikao cha wataalam wa mifugo wanaohusika na ukusanyaji maduhuli ya serikali kilichofanyika Jijini Dodoma.
…………………………………………………………..
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki ametoa maelekezo manne kwa wataalam wa mifugo wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwa lengo la kuhakikisha wanafikia lengo lililowekwa.
Waziri Ndaki ametoa maelekezo hayo kwenye kikao na wataalam hao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Royal Village ambapo aliwaeleza kuwa mwenendo wa ukusanyaji wa maduhuli ya serikali sio mzuri kwani kati ya bilioni 50 zilizokusudiwa kukusanywa ni bilioni 13.9 ndio zimekusanywa.
Katika kikao hicho taarifa za ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ziliwasilishwa kwa kila kituo ambapo pia changamoto ziliwasilishwa na kujadiliwa namna gani ya kuweza kukabiliana nazo ili kuhakikisha ukusanyaji wa maduhili unafikia malengo yaliyowekwa
Akizungumza na wataalam hao Waziri Ndaki amesema kuwa wizara iliamua kuunda timu ya ufuatiliaji kwa lengo la kuangalia hali ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwenye minada na vituo vilivyo chini ya wizara. Timu hiyo ilibaini changamoto mbalimbali na kutoa mapendekezo ambayo yatasaidia kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Baada ya majadiliano ya taarifa zilizokuwa zimewasilishwa, Waziri Ndaki aliwaeleza wataalamu hao kuwa ni lazima wajipange vizuri kuhakikisha wanafikia malengo ya ukusanyaji maduhuli ya serikali kama walivyo pangiwa.
“Viongozi tutaendelea kuwafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha malengo ya ukusanyaji maduhuli ya serikali yanatimizwa na kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu kwa makusudi hatua zitachukuliwa dhidi yake,” alisema Waziri NDAKI
Pia amemueleza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya Mifugo, Bw. Tixon Nzunda kuwasiliana na Katibu Mkuu TAMISEMI ili kuhakikisha Halmashauri zilizotumia fedha za makusanyo ya maduhuli za wizara zikiweno za Halmashauri Mvomero, Tarime na Manyoni zinarejesha fedha hizo.
Lakini pia wataalam wametakiwa kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na kwa kujitolea ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yanatimizwa. Waziri Ndaki amewaeleza wataalam hao kuwa katika muda wao wa utumishi ndani ya sekta ya mifugo ni lazima waache alama ikiwemo ya ukusanyaji mzuri wa maduhuli. Wataalam hao wametakiwa kuwa wabunifu katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuhakikisha wanasimamia sheria, kanuni, miongozo na taatibu zilizowekwa.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Mifugo, Bw. Tixon Nzunda amewataka wataalam hao kwenda kufanya kazi kwa uadilifu lakini pia watalazimika kuwajibika kutokana na matendo yao kwenye suala la ukusanyaji wa mapato. Vilevile amewataka kuhakikisha wanakusanya mapato katika maeneo yao na kucha tabia ya udanganyifu kwani hatua zitachukuliwa dhidi yao. Adiha, amewataka wataalam hao kuwasilisha taarifa za makusanyo kila mwezi.
Pia amemshukuru Waziri kwa uamuzi wake wa kuitisha kikao hicho kwani kimesaidia kwa kuwawezesha wataalam wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli Tanzania Bara kukaa kwa pamoja kujadili changamoto walizonazo na kutoka na mkakati wa pamoja ili kuhakikisha ukusanyaji wa maduhuli unakwenda vizuri.
Mkuu wa Mnada wa Ipuli mkoani Tabora, Fred Senyagwa amesema kuwa watakwenda kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Waziri ili kuhakikisha wanakusanya maduhuli kulingana na malengo yaliyowekwa.
Kaimu Mkuu wa Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo – Iringa, Bw. Rajon Deule amesema kuwa sababu ya kituo chao kufanya vizuri ni kwamba Kanda yao wamekuwa wakifanya vikao vya mara kwa mara ambavyo huwa wanajadili changamoto wanazokutana nazo na kujiwekea mikakati ya namna ya kukabiliana nazo. Kwa kutumia njia hiyo imewasaidia kuweza kukusanya maduhuli ya serikali vizuri.
Kikao hicho cha wataalam kimefanyika kwa lengo la kuwakutanisha wataalam wa mifugo wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ili waweze kujadili changamoto na mikakati itakayowezesha sekta ya mifugo kutimiza malengo ya ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.