Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ya kutwa ya Mbinga iliyopo katika Halmashauri ya Mji Mbinga wakati wa ziara yake ya kukagua mwitiko wa wanafunzi kuripoti shuleni.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Mbinga waimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge aliyetembelea katika shule hiyo kwa ajili ya kuangalia mwitikio wa wanafunzi waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2022,hata hivyo Jenerali Ibuge akuridhishwa na idadi ya wanafunzi walioripoti katika shule walizipangiwa katika wilaya hiyo ambapo kati ya wanafunzi 2,361 walioachaguliwa kuanza kidato cha kwanza ni 551 tu ndiyo walioripoti.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda akizungumza jana na wanafunzi na walimu wa shule ya Sekondari Mkinga Halmashauri ya Mji Mbinga wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kukagua mahudhurio ya wanafunzi wa kidato cha kwanza walioachaguliwa kuanza elimu ya sekondari mwaka 2022 wilayani humo,kulia Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo,wa pili kulia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mbinga Grace Quintine na kushoto mjumbe wa bodi ya shule Daniel Chindengwike.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Azazi Mangosongo kushoto,akimsikiliza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge wakati Mkuu wa mkoa alipotembelea shule ya Sekondari ya kutwa Mbinga kwa ajili ya kukagua mwitikio wa mahudhurio ya wanafunzi wa kidato cha kwanza waliochaguliwa kuanza elimu ya Sekondari katika wilaya hiyo mwaka 2022,hata hivyo Jenerali Ibuge hakuridhishwa na mahudhurio ya wanafunzi katika shule walizopangiwa,wa pili kulia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mbinga Kelvin Mapunda.
……………………………………….
Na Muhidin Amri,
Mbinga
KATI ya wanafunzi 2,361 waliotakiwa kuripoti kuanza masomo ya kidato cha kwanza wilayani Mbinga mkoani Ruvuma ni wanafunzi 551 sawa na asilimia 23.3 tu ndiyo walioripoti kwenye shule walizopangiwa.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, ameagiza ndani ya wiki hii wanafunzi wote waliobaki wawe wamefika shule na kuwaagiza watendaji wa vijiji na kata kuanza msako wa watoto wote waliobaki nyumbani licha ya shule kufunguliwa.
Brigedia Jenerali Ibuge,ametoa agizo hilo jana alipotembelea shule ya sekondari ya kutwa Mbinga na Mkinga katika Halmashauri ya Mji Mbinga wilayani Mbinga, kwa ajili ya kukagua mwitikio wanafunzi wa kidato cha kwanza wanaotakiwa kuanza masomo ya sekondari mwaka 2022.
Mkuu wa mkoa alisema, wazazi na walezi wa watoto ambao bado hawajaripoti kwenye shule wanatakiwa kuelewa kuwa, suala la watoto kwenda shule sio hiari bali ni lazima na hakuna maana kama serikali imetumia nguvu na fedha nyingi kujenga madarasa lakini watoto hawapelekwi shule.
“suala la wazazi na walezi kupeleka watoto wao shule sio hiari ni lazima,sisi kama viongozi ni muhimu tusimamie jambo hilo,watendaji wa vijiji,kata,Wakurugenzi wa Halmashauri na wakuu wa wilaya hakikisheni hakuna mtoto anayebaki nyumbani na kushindwa kwenda shule kwa namna yoyote ile”alisema Ibuge.
Akizungumzia ujenzi wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa kwa fedha za mpango wa maendeleo na ustawi wa Taifa ikiwa ni mkopo kutoka Shirika la fedha Duniani(IMF),Ibuge amewapongeza viongozi wa wilaya hiyo kwa kusimamia vyema ujenzi wa madarasa ambayo yamekamilika kwa asilimia 100.
Amewataka wanafunzi,walimu na jamii ambako madarasa hayo yamejengwa kuhakikisha wanayatunza na kuyatumia kwa kazi iliyokusudiwa ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na kuinua hali ya elimu katika mkoa wa Ruvuma.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziz Mangosongo alisema, wanafunzi ambao hadi sasa bado hawajaripoti shule ni 1,810 sawa na asilimia 76.67.
Akiwa katika shule ya Sekondari Mkinga inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi,Ibuge amekabidhi mifuko 100 ya saruji kama mchango wake kwa shule hiyo ili kuboresha miundombinu ya elimu hususani ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Alisema,lengo la msaada huo ni kuwatia moyo wanafunzi na walimu wa shule hiyo kufuatia ufaulu mzuri katika mitihani mbalimbali na kuwapongeza walimu kwa mkakati wao wa kuondoa daraja la 3 na4 katika matokeo ya mitihani mbalimbali.
Alisema, suala la maendeleo halina chama wala kabila na kuwaomba wadau wa ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma kuona umuhimu wa kuisaidia shule hiyo ili iendelee kufanya vyema kitaaluma.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Jonas Mbunda ambaye ni miongoni mwa watu waliosoma katika shule hiyo,amemshukuru Mkuu wa mkoa kwa msaada huo ambao unakwenda kutatua changamoto ya vyumba vya madarasa.
Mbunda ametoa wito kwa walimu, kusimamia taaluma na maendeleo ya shule na wanafunzi kuhakikisha wanasoma kwa bidi na kutimiza ili watimize malengo yao.
Pia amemshukuru Rais Samia Hassan kwa uamuzi wa kutoa fedha zilizotumika kujenga vyumba vya madarasa katika wilaya hiyo ambayo yamepunguza changamoto ya watoto kubanana katika chumba kimoja.
Makamu Mkuu wa shule Fabian Kumburu alisema, kwa miaka mitano mfululizo shule imeweza kuondoa daraja F na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na masomo ya kidato cha tano.
Alisema, katika matokeo ya mitihani ya Taifa kidato cha nne kuanzia mwaka 2018-2021 ufaulu ni asilimia 100 na kwa mara ya kwanza wamefanikiwa kuondoa daraja la nne katika matokeo ya kidato cha nne.