Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtakaakizungumza na waandishi wa habari leo Januari 21,2022 wakati akitoa taaarifa kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Sheria Kitaifa yatakayofanyika Siku ya Jumapili kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo Januari 21,2022 wakati akitoa taaarifa kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Sheria Kitaifa yatakayofanyika Siku ya Jumapili kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Naibu Msajili Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dodoma, Benard Mpepo,akielezea siku ya Wiki ya Sheria Kitaifa yatakayofanyika Siku ya Jumapili kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
……………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ally Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi maadhimisho ya Wiki ya Sheria Kitaifa yatakayofanyika Januari 23,2022 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 21,2022 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka,wakati akitoa taaarifa kwa vyombo vya habari kuhusu maadhimisho hayo ya kitaifa.
“Natumia nafasi hii kuwajulisha kuwa sherehe za maadhimisho ya Wiki ya Sheria Kitaifa zitafanyika kwenye mkoa wetu wa Dodoma, makao makuu ya nchi kuanzia tarehe 23 Januari hadi 29 mwaka huu. Aidha sherehe za siku ya sheria nchini zitafanyika pia kwenye mkoa wetu tarehe 1 Februari 2022,”amesema Mtaka
Mtaka amesema kuwa uzinduzi wa maaadhimisho ya Wiki ya Sheria utafanyika kesho ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ally Mwinyi.
Amesema sherehe hizo za uzinduzi zitaanza kwa zoezi la matembezi yatakayoanza saa12:00 asubuhi katika viwanja vya kituo jumuishi Cha haki na kuiishia kwenye viwanja vya Nyerere Square ambapo sherehe za uzinduzi itafanyika.
“Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yatafanyika kwa wiki nzima yakijumuisha shughuli za uzinduzi wa bendera ya mahakama, uzinduzi wa mahakama ya wilaya ya Chemba, uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa jingo la makao makuu ya mahakama ya Tanzania pamoja na uzinduzi wa mahakama ya wilaya ya Bahi,”amesema Mtaka
RC Mtaka amesema kuwa maadhimisho ya kilele cha siku ya sheria kitafanyika katika Viwanja vya Chinangali Februari mosi ambapo mgeni rasami atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hata hivyo Mtaka amezitaka taasisi zote za Serikali,binafsi,makundi mbalimbali,wadau wote wa mahakama na wananchi wote wa mkoa wa Dodoma kwa ujumla na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kwenye sherehe hizo za maadhimisho ya wiki ya Sheria kitaifa.
“Pia elimu sheria ya haki za watoto, wanawake na ushauri wa mambo mbalimbali, elimu juu ya kamati za maadili kwa maafisa wa mahakama ngazi ya mkoa na wilaya zitatolewa,”amesema
Kwa upande wake, Naibu Msajili Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dodoma, Benard Mpepo,amesema kuwa kwenye maadhimisho hayo kutakuwa na uzinduzi wa majarida na sheria mbalimbali zinazohusu mahakama zitakazofanywa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
”Tunaushukuru Mkoa wa Dodoma kwa kukubali maadhimisho hayo kufanyika hivyo tunawaomba wakazi wa Mkoa wa Dodoma na wale wa mikoa ya jirani kuhudhuria katika maadhimisho hayo ya wiki moja kwa kuwa yataambatana utoaji masaada wa kisheria kwenye masula mbalimbali ikiwemo mirathi, ndoa, talaka na migogoro mbalimbali”