Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma Bw. Sosthenes Kibwengo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Januari 20,2022 jijini Dodoma.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma Bw. Sosthenes Kibwengo,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)wakati akizungumza nao leo Januari 20,2022 jijini Dodoma.
………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma Bw. Sosthenes Kibwengo,amesema kuwa kwa kushirikiana na wadau wamefatilia ujenzi wa madarasa yaliyojengwa kwa fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko- 19 na kuridhishwa na ujenzi huo ambao umetekelezwa vizuri .
Hayo ameyasema leo Januari 20,2022 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa Habari Kibwengo, amesema kuwa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa madarasa umesimamiwa kikamilifu.
Pia amesema kuwa wameichunguza miradi minne na kubaini kuwa Kati ya miradi minne, miradi mitatu kati yake ilikutwa na dosari ndogo ndogo, ambazo zilijadiliwa na kurekebishwa.
Pia amesema kuwa wamekamilisha ufuatiliaji wa miradi minne iliyokuwa imekataliwa kuzinduliwa na Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021.
”Kati ya miradi hiyo minne, miradi mitatu kati yake ilikutwa na dosari ndogo ndogo, ambazo zilijadiliwa na kurekebishwa, lakini kwenye mradi mmoja inaonekana kuna malipo yaliyofanyika bila ya kazi husika kutekelezwa, hivyo tunashirikiana na halmashauri husika kufuatilia marekebisho ya dosari hiyo.”ameeleza
Kibwengo amesema kuwa pamoja na madarasa hayo pia walikagua miradi 596 ya ujenzi yenye thamani ya zaidi ya sh.bilion 20 ambapo walishauri wahusika kuboresha maeneo yaliyokuwa na changamoto.
“Tunawakumbusha watendaji na wananchi kwa ujumla kuzingatia kwamba vifaa vya ujenzi katika miradi inayotekelezwa kwa njia ya manunuzi ya force account vinapaswa kununuliwa kwa kuzingatia bei ya soko ili thamani ya fedha ifikiwe,”amesisitiza
Aidha Bw.Kibwengo amesema kuwa kupitia dawati la uchunguzi wamepokea jumla ya
taarifa 106 ambapo taarifa za rushwa 58 tu zisizohusu rushwa zilikuwa
48 na taarifa 58 zilizohusu rushwa zimeshuhulikiwa kwa njia ya uelimishajina uzuiaji rushwa.
Amesema kuwa taarifa zilizohusu rushwa zilishughulikiwa kwa njia ya uzuiaji rushwa, uelimishaji pamoja na uchunguzi ambapo hadi sasa uchunguzi wa majarida 19 umekamilika na mashauri matano yamefunguliwa mahakamani.
Hata hivyo ameeleza kuwa kati ya taarifa 48 ambazo hazikuhusu rushwa nane zilihamishiwa Idara nyingine, taarifa 40 watoa taarifa walielimishwa na kushauriwa ni wapi mahali sahihi pa kuwasilisha malalamiko yao.
“Pia tulipokea taarifa 106 zilizohusu sekta mbali mbali ikiwemo serikali za mitaa, vijiji, kata na halmashauri ambapo zilikuwa 36, sekta ya ardhi 19, elimu, 11, mahakama tisa, afya saba, fedha tano na sekta nyinginezo 19,”ameeleza
Pia amesema kuwa katika eneo la uelimishaji umma kuhusu mapambano dhidi ya rushwa walifanikiwa kufanya mikutano 47 ya hadhara, semina 90, onesho moja, na kutembelea klabu 121 za wapinga rushwa shuleni na vyuoni.
Ameeleza kuwa baadhi ya mikutano ilifanyika kwa utaratibu wa TAKUKURU inayotembea ambapo kwa kutumia gari ya matangazo waliwahamasisha wafanyabiashara kuzingatia kanuni na sheria za uendeshaji wa biashara.
Hata hivyo amewataka wafanyabiashara kutambua umuhimu na wajibu wa kulipa kodi, kutotoa au kushawishi kutoa rushwa na kutoa taarifa kwa TAKUKURU pindi wanapokutana na watumishi wanaotaka kujihusisha na rushwa.
“TAKUKURU kwa kushirikiana na skauti inazingatia umuhimu wa makuzi mema kwa vijana ili kuwajenga katika uadilifu, uzalendo na uwajibikaji ambazo ni silaha zitawafanya wawe wananchi na watendaji makini wasio na hulka za ubinafsi ambazo huzalisha matumizi mabaya ya madaraka na ubadhilifu wa fedha za umma,”amesema Kibwengo