Mawaziri wa Mambo ya Nje wa
Tanzania na Uganda walifungua Mkutano wa Nne wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati
ya nchi hizo mbili unaofanyika leo tarehe 19 Januari 2022 jijini Kampala, Uganda.
Mkutano huu wa siku moja
ulitanguliwa na Mkutano Ngazi ya Wataalamu uliofanyika tarehe 17 Januari 2022
na kufuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 18 Januari 2022.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano
huu unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) ambaye ameambatana na Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.), Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mhandisi Geodfrey
Kasekenya(Mb.), Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud
Kigahe (Mb.), Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Antony Mavunde (Mb.) na Naibu Waziri
Wizara ya Nishati, Mhe. Steven Byabato (Mb.).
Mkutano wa Nne umejadili na
kutathimini masuala mbalimbali ya utekelezaji kwenye maeneo ya ushirikiano
yaliyokubaliwa baina ya nchi hizi. Maeneo hayo ni pamoja na; Siasa na
Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Fedha
na Uchumi, Nishati, Habari na Mawasiliano, Kilimo, Maendeleo na ujenzi wa
Miundombinu, Elimu na Mafunzo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo
na Uvuvi, Maji na Mazingira, Afya na Elimu.
Akifungua Mkutano huo Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata
Mulamula ameishukuru Jamhuri ya Uganda kwa mapokezi mazuri ya kidugu na uratibu mzuri wa mkutano huo.
Pia, akaeleza imani aliyonayo
kwa wajumbe wa mkutano huu ambao walijadili na kutoa maamuzi katika maeneo
mbalimbali ya utekelezaji yaliyowasilishwa kwa ustawi wa mataifa haya, sambamba
na kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano kupitia majadiliano hayo.
“Serikali zetu zimejikita katika kuhakikisha vikwazo vya biashara
vinatatuliwa na hili linafanyika mara kwa mara katika ngazi zote za utekelezaji
na maamuzi”, alisema Balozi Mulamula
Pia akafafanua kuwa kupitia
ziara za viongozi wetu wakuu Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mhe. Yoweri Kaguta Museven, Rais wa Jamhuri ya Uganda
changamoto na tozo mbalimbali za kibiashara zilitatuliwa ili kukuza na kuinua
urali wa biashara baina ya Tanzania na Uganda.
Kwa upande wa Waziri wa Mambo
ya Nje wa Uganda, Mhe. Jen. Jeje Odongo alieleza kuwa Mkutano huu utajadili na kufanya makubaliano katika sekta mbalimbali za ushirikiano zitakazosainiwa katika nyakati tofauti kwa lengo la kufungua maeneo
mapya ya ushirikiano ili kuendelea kuimarisha ushirikiano na kutumia fursa
zilizopo kwa manufaa ya wananchi wa Nchi hizi mbili.
Aidha, akafananua mkutano huu
utajadili hali ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika nchi
hizi mbili pamoja na mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaojengwa na
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Reli hii ya kisasa (SGR)
itapunguza adha za usafiri kwa Nchi za Afrika Mashariki sambamba na
kuziunganisha nchi za ukanda huo na kupunguza gharama za kibiashara”, alisema
Jen. Odongo.
Kwa pamoja viongozi hao
walizitaka sekta zilizopo katika maeneo hayo ya ushirikiano kuhakikisha
wanatekeleza na kutatua kwa wakati masuala yote ya kitendaji ili kuruhusu sekta
hizo kustawi kiuchumi na kuinua maisha ya Wananchi.
====================================================================
Mhe. Waziri Mulamula pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax wakifatilia majadiliano ya mkutano huo. |
Mhe. Jen. Odongo, Mawaziri kutoka katika sekta za ushirikiano na ujumbe wa Wataalamu wakifuatilia majadiliano. |
Kutoka kushoto Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Antony Mavunde na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Steven Byabato wakifuatilia Mkutano. |
Kutoka kulia Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Mhandisi Geodfrey Kasekenya na Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe wakifuatilia majadiliano. |
Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Balozi Mulamula na Jen. Odongo wakionesha Hati za Muhtasari wa Makubaliano walizosaini mara baada ya kukamilisha majadiliano ya mkutano huo. |
Picha ya Pamoja Mawaziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Balozi Mulamula na Jen. Odongo |
Picha ya Pamoja Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wengine wa kisekta walioshiriki kwenye majadiliano ya Mkutano huo. |