Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akipata maelezo kuhusu kitalu cha miche cha Kikundi cha Vijana Wakereketwa wa Mazingira (KIVIWAMA) kilichopo Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro alipofanya ziara ya kukagua shughuli za mazingira
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na wanakikundi cha Upendo kinachohusisha na shughuli za kuotesha miche kilichopo Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro alipofanya ziara ya kukagua shughuli za mazingira
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akipokea mche wa mti aliozawadiwa na wanakikundi cha Upendo kilichopo Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro alipofanya ziara ya kukagua shughuli za mazingira Januari 18, 2022.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
………………………………………………………………….
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Jafo amezielekeza halmashauri kuhakikisha zinaweka bajeti ya kutosha kwa ajili ya utunzaji na usimamizi wa mazingira.
Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo Januari 18, 2022 wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua shughuli mbalimbali za mazingira katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Akitembelea na kukagua vikundi mbalimbali vinavyojihusisha na uoteshaji wa miche alionesha kuridhishwa na namna wanavyoshiriki kikamilifu katika kusukuma mbele agenda ya mazingira.
Alitoa wito kwa halmashauri nchini kuvitumia vikundi katika suala la uhifadhi wa mazingira hatua itakayosaidia kupata miche ya kupanda katika taasisi na maeneo mbalimbali.
Pia Waziri Jafo alisema kuwa endapo halmashauri zitashirikiana na vikundi hivyo kwa kuvitengea bajeti itakuwa ni njia mojawapo ya kupunguza changamoto ya uhaba wa miche.
“Tukiviwezesha vikundi vya kimazingira vinapata mitaji ya kuotesha miche mingi zaidi na sisi kama Serikali tunaenda kununua miche kwao na kuipanda katika taasisi zetu kama mnavyofanya watu wa Moshi mna vikundi 52 ambavyo mtaweza kuvitumia na wakati huo mazingira yetu yanakuwa mazuri,” alisema.
Akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya mazingira Afisa Mazingira wa Manispaa ya Moshi, Bi. Benedicta Mtei alisema manispaa hiyo ina vitalu 52 vya watu binafsi na vikundi ambavyo vimejikita katika uoteshaji wa miche.
Alisema manispaa haina kitalu lakini wamejikita katika kutoa elimu na kuwahamasisha wanachama wa vikundi hivyo mbinu za kujipatia kipato kupitia miradi ya uoteshaji wa miche.
Bi. Mtei aliongeza kuwa vikundi hivyo huotesha miche takriban milioni 1.5 ikiwemo ya miti ya matunda, kivuli na asili ambayo huiuza kwa taasisi mbalimbali na watu binafsi na kupandwa.
Awali Waziri alitembelea alifanya ziara katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA) ambapo aliwapongeza kwa jitihada za kuhifadhi mazingira katika eneo la hifadhi hiyo ikiwemo.
Alihamasisha wadau mbalimbali kusaidia katika jitihada za kuhifadhi eneo hilo kwa kutokata miti ovyo ambapo alisema endapo hazitafanyika jitihada hizo kutaleta athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema kampeni ya upandaji miti milioni 1.5 katika kila wilaya nchini inayohusisha pia wanafunzi itasaidia kulinda hifadhi ya mlima huo na kunusuru nchi na mabadiliko ya tabianchi.