Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na Watoto wanaoishi na kulelewa katika Makao ya Taifa ya Watoto yaliyopo Kikombo mkoani Dodoma.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akizungumza mbele ya Watoto na watumishi katika Makao ya Taifa ya Watoto yaliyopo Kikombo mkoani Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainabu Chaula akifafanua jambo wakati akizungumza na Watoto na watumishi katika Makao ya Taifa ya Watoto yaliyopo Kikombo mkoani Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju akielezea jambo wakati akizungumza na Watoto na watumishi katika Makao ya Taifa ya Watoto yaliyopo Kikombo mkoani Dodoma.
Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara, Wakuu wa Taasisi na Vyuo na baadhi watumishi waliopo katika Makao ya Taifa ya Watoto yaliyopo Kikombo mkoani Dodoma wakimsikiliza Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alipotembelea Makao hayo.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM
……………………………………………………..
Na WMJJWM Dodoma
Serikali imezitaka Taasisi za Ustawi na Maendeleo ya Jamii nchini kuimarisha ushirikiano na jamii zinazowazunguka ili kuhamasisha, kuelimisha na kubuni mbinu inayowezesha jamii hizo kujiendeleza na kuepusha watoto na vijana kukimbilia mijini na kujiingiza kwenye ajira zisizo rasmi na kuharibu matarajio yao ya mbeleni.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), wakati alipozuru Makao ya Taifa ya kulelea watoto Kikombo, katika Mkoa wa Dodoma, katika ziara hiyo alifuatana na Menejimenti ya Wizara pamoja na Wakuu wa Vyuo na Taasisi za Maendeleo ya Jamii nchini.
“Siku ya jumatatu tulikutana na watoto waishio kwenye mazingira hatarishi miitaani hapa Dodoma na katika kuwasilikiza wapo baadhi yao unawaona kabisa wanao mwelekeo lakini wamekosa wa kuwaongoza njia sahihi hivyo wameamua kutoroka majumbani na kukimbilia mijini” amesema Dkt. Dorothy Gwajima. Na kuongeza “lakini kama vyuo vyetu vikiliona hili na kuisaidia jamii tunaweza kupunguza wimbi la watoto kukimbilia mijini alisisitiza Waziri Gwajima. Akirejea taarifa ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inayokadiriwa kuwa, jumla ya watoto milioni 2.5 walikuwa wanaishi na kufanya kazi mitaani kufikia mwaka huo sawa na asilimia 12 ya watoto wote nchini.
Dkt. Gwajima aliongeza kusema kuwa, mpango wa serikali ni kuwaondoa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi na kuwarejesha kwenye mazingira bora kupitia makao ya watoto nchini kote ambapo kwa sasa kuna jumla ya vituo 468 huku akimwagiza, Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Zainab Chaula, kushirikiana na wamiliki wa vituo binafsi na kufanya tathmini ya uwezo na utayari wa vituo vyote jinsi gani vinaweza kuwa sehemu ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amewaasa Maafisa Ustawi wa Jamii katika Makao hayo, kuhakikisha wanawalea Watoto waliopo hapo kwa kuzingatia maadili, taratibu na miongozo mbalimbali ya Malezi na Makuzi kwa Mtoto.
“Jukumu letu hapa nikutoa Malezi ambayo mtoto angeweza kuyapata akiwa kwa mzazi wake, hivyo sisi kama jamii tulioamua kubeba dhamana hii lazima tuoneshe mapenzi mema kwa watoto hawa ili waweze kujiona wana thaminiwa na jamii yao” alisema Mwanaidi.
Naye Naibu Katibu Mkuu. Bw. Amon Mpanju alisisitiza juu ya Watoto wenye changamoto mbalimbali za ulemavu kuwa waweze kupatiwa huduma stahiki kwa kuwaongezea ujuzi na maarifa walezi ili waweze kuwalea Watoto hao kulingana na miongozo stahiki.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Katibu Mkuu Dkt. Zainabu Chaula, alisema amepokea maelekezo hayo kwa utekelezaji na ameahidi kusimamia na kuhakikisha kuwa, Makao ya Taifa ya Watoto na mengine yote nchini yanajielekeza kwenye kutoa Watoto watakaoweza kujitegemea na kufika mbali kwa kupatiwa stadi mbalimbali ili waweze kuchangia katika uchumi na maendeleo ya Taifa.
Awali akitoa taarifa ya kituo hicho, Afisa Mfawidhi wa Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Vivian Kaiza, alisema maono ya kituo hicho ni kuwa cha mfano kitaifa katika kuwalea Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kufanya kazi zisizo rasmi kwa kuwapatia Malezi na Makuzi ya stadi za kazi kwa lengo la kujitegemea baadae.
Hivi sasa Serikali ipo katika jitihada za kuhakikisha inapata ufumbuzi wa kuondokana na tatizo la Watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani ili kuwapatia Watoto hao Malezi na Makuzi Bora pamoja na stadi za maisha.